MCHAMBUZI wa soka nchini kupitia kipindi cha Krosi Dongo cha Global TV ameushauri uongozi wa Yanga kufanya mazungumzo na uongozi wa Simba ili kutafuta namna ya kukamilisha dili la kumsajili kiungo mshambuliaji raia wa Ghana Bernard Morrison.
Simba SC ilitangaza kumpa mapumziko mchezaji wake Bernard Morrison hadi mwisho wa msimu huku pia ikimtakia mafanikio mema na kumshukuru kwa mchango wake ndani ya klabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimethibitishwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo Ahmed Ally ni kwamba Morrison ana mkataba na klabu hiyo unaotarajiwa kumalizika mwezi Agosti hivyo kama kuna klabu yoyote ile inahitaji huduma ya Morrison ni wazi italazimika kuingia katika meza ya mazungumzo na klabu ya Simba au isubiri hadi kutamatika kwa mkataba wake.
Jembe ameishauri Yanga kutoa Milioni 20 kumsajili Bernard Morrison kutoka Simba SC
Kupitia kipindi cha Krosi Dongo Saleh Jembe amesema:
“Yanga wanaweza kusema sisi tunaweza kumkosa lakini hata nyie baada ya mwezi mmoja atakuwa siyo wenu kwahiyo mnaonaje kama mkichukua hata milioni 20 halafu mkatuachia sisi tukamuwahi ili tuweze kumuingiza kimataifa, Ingekuwa hizi klabu zinaweza kuwa na mazungumzo mazuri yenye maelewano hakuna haya mambo ya machagizo ya kuzifanya timu zionekane zina uadui na nini, ingeweza kuwa ni jambo rahisi sana kwasababu ukiangalia Simba haiwezi kuwa naye ndani ya mwezi mmoja.”
Bernard Morrison mchezaji wa Simba SC
Simba na Yanga zote zinaendelea na harakatai zao za usajili ili kuimarisha vikosi vyao ambapo kwa Yanga tayari imeshamtambulisha mshambuliaji raia wa Zambia Lazarous Kambole aliyetokea klabu ya Kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini huku Simba nao wakimtambulisha pia Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Zambia Moses Phiri kutoka klabu ya Zanaco ya nchini humo