Yanga yavamia anga za wakubwa, yawatunishia Berkane, Fenerbahce


YANGA imeingia kwenye vita ngumu na klabu za Uarabuni. Ya kwanza ni dhidi ya RS Berkane, lakini vilevile TP Mazembe inahusishwa.

Vita nyingine ni dhidi ya Fenerbahce na Besiktas za Uturuki. Na hiyo yote ni juu ya wachezaji watatu Wakongomani, Glody Makabi Lilepo, Tuisila Kisinda pamoja na mzawa Saimon Msuva.

Yanga imepania kufumua na kuzisuka upya safu zake za ushambuliaji wa pembeni ikilenga haswa kufanya vizuri msimu ujao katika Ligi ya Mabingwa barani Afrika inayotarajiwa kuanza Agosti 12, mwaka huu.

Makabi alikuwa chaguo lao la kwanza, lakini punde Berkane na Mazembe wakaingilia mazungumzo na kuongeza mzigo kwa staa huyo wa AS Vita, ila Yanga wakaendelea kumshawishi kupitia mastaa waliopo Jangwani kina Fiston Mayele kuwa atacheza haswa kikosi cha kwanza.


 
Habari za ndani zinasema kwamba Yanga wameamua kutulia na hawatumii tena nguvu kubwa kusukuma dili hilo na mezani wamebakiwa na majina mawili tu.

Katika majina hayo moja ni la Msuva wa Wydad Casablanca ambaye bado yupo kwenye mgogoro na timu yake hiyo na jingine la Kisinda wa Berkane ambaye hata Mazembe nao wanamtaka japo kwa mkopo, kwani bado ana mkataba wa miaka miwili huko Morocco.

Habari za uhakika zinasema kwamba Tuisila mwenyewe ndiye aliyeomba vigogo wa Yanga kurejea ingawa bado hawajakubaliana na ombi lake kutokana na kile walichojifunza kwa Clatous Chama aliyerejea Simba na Heritier Makambo Yanga wanaoonekana kama wameshuka ubora tofauti na awali. Chama alirejea Simba akitokea Berkane ilhali Makambo alikuwa Horoya FC.


Habari zinasema akili za Yanga kwa sasa zipo kwa Msuva ambaye bado ni mgumu kufanya uamuzi kwani wakala wake anataka kumpeleka Fenebahce au Besiktas ambazo zimeonyesha nia na zina mzigo wa maana mezani licha ya kwamba bado anasikilizia kesi yake na Waydad Casablanca. Yanga wameshafanya mazungumzo mara kadhaa na Msuva na kocha Nasreddine Nabi amemuweka kama chaguo la kwanza kwenye usajili wa mawinga na hata kuanza kikosi cha kwanza. Habari zinasema Nabi amejilipua kwa Msuva baada ya kumuona kwenye mechi kadhaa na vilevile anaamini atatumia mapenzi yake kwa Yanga kufanya makubwa Ligi ya Mabingwa ambako wamepania kuingia kwa miguu miwili.

Nabi aliliambia Mwanaspoti juzi kwamba, anatamani kuwa na Msuva kikosini na alifurahi alipoingia kwenye vyumba vya kubadilishia Yanga ilipocheza na Coastal Union jijini Dar es Salaam, ingawa hajataka kuweka wazi dili hili limefikia wapi.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad