Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans wanaendelea na maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Coastal Union utakaopigwa mwishoni mwa juma hili, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Afisa Habari wa Young Africans Hassan Bumbuli amesema, maandalizi ya kikosi chao yapo katika hali zuri, na wanatarajia kuona mambo yakiendelea kuwanyookea katika mchezo huo.
Amesema bado lengo lao ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa msimu huu pasina kupoteza mchezo wowote, hivyo Benchi la Ufundi linafanya kazi yake kwa kuzingatia viwango vya ubora, kama ilivyokua kabla ya kusimama kwa Ligi kupisha michezo ya Kimataifa.
Young Africans: Fiston Mayele hauzwi
Hata hivyo Bumbuli amesema kiungo Zawadi Mauya anaendelea kukosa sehemu ya maandalizi ya kikosi chao, kufuatia kuwa majeruhi, hivyo hana uhakika wowote wa kucheza dhidi ya Coastal Union.
“Kikosi kinaendelea na maandalizi yake vizuri, wachezaji wote waliopo kambini wanaendelea vizuri isipokuwa Zawadi Mauya, ambaye ni majeruhi. Mchezaji huyu amekua na majeraha tangu tulipocheza dhidi ya Biashara United Mara kule Mwanza, na hakuna uwezekano wowote wa kupona kwa haraka na akawa sehemu ya mchezo wetu dhidi ya Coastal Union.”
“Madaktari wameshampeleka hospitali kwa ajili ya kumfanyia vipimo, na kulingana na taratibu zinazoendelea ni kwamba ataendelea kuwa nje ya uwanja kwa majuma mawili Zaidi.”
“Kwa upande wa maandalizi ya timu, mambo yapo vizuri na tuna imani kubwa sana tutakwenda kucheza kwa umakini mkubwa dhidi ya Coastal Union, tumecheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Friends Rangers na tumewafunga mabao 8-0, hivyo tupo vizuri,”
“Hii inaonyesha wachezaji wetu wapo tayari, wameonyesha kuwa katika hatua nzuri ya kwenda kupambana, wale ambao wapo kwenye timu ya taifa wataungana na wenzao wakati wowote kuanzia sasa, tayari kwa mpambano wetu dhidi ya Coastal Union.” amesema Bumbuli
Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 64 baada ya kucheza michezo 26 huku wapinznai wao Coastal Union wakishika nafasi ya sita kwa kufikisha alama 34 zilizotokana na michezo 26 waliocheza hadi sasa.
Timu hizo zitakutana tena jijini Arusha Julai 02 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kwenye mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanznaia Bara ‘ASFC’.