YANGA imekamilisha usajili wa mshambuliaji kutoka Asec Mimosas, Stephano Ki Aziz wakati huo huo taarifa za ndani ya klabu hiyo zinaeleza imekamilisha usajili wa Benard Morrison kutoka Simba.
Morrison atachelewa kutambulishwa kutokana na mkataba wake na Simba kumalizika Agosti 30, mwaka huu, siku chache kabla ya msimu ujao kuanza wakati huo hadi mechi ya Ngao ya Hisani itakuwa imechezwa.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza Morrison ametuma maombi kwa njia mbalimbali, ujumbe mfupi wa maneno wa simu, barua pepe, kupiga simu na kuzungumza na viongozi wa juu ili wampe barua inayoonyesha yupo huru.
Morrison amewaomba mabosi wake ambao hivi karibuni walimtakia kila la heri kwenda kutatua matatizo ya kifamilia kumpatia barua hiyo akieleza kwamba kuna timu kutoka nchi mbalimbali zinamtaka.
Kiongozi mmoja wa Simba alisema Morrison amewafuata na kuwaeleza amepata ofa kutoka timu kama Raja Casablanca ya Morocco na Qatar.
“Baada ya kutueleza timu zinazotaka kumsajili akatuomba tumpatie ‘release latter’ ili akamalizane nao na kuanza maisha mapya huko. Tumemjibu hizo timu zinazomtaka zitutumie barua rasmi ya kuonyesha nia hiyo nasi tutakuwa tayari kuwapatia,” alisema kiongozi huyo.
“Kama kweli hizo timu zikitutumia barua rasmi tumemueleza Morrison tutawapatia hiyo barua na akatafute maisha mapya huko anapotaka kwenda ila maombi ya maneno yake tu hatutampatia hadi siku ya mwisho ya mkataba wake utakapofikia.
“Hapaswi kutumia nguvu kubwa ya kutaka hiyo barua tutampatia muda ukifika kwani tunafahamu kwanini analazimisha hivyo kuna timu amemalizana nayo hapa nyumbani.”
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema wao walimpa ruhusa Morrison kwenda kushughulikia masuala yake ya kifamilia ndio maana wanaishi vizuri na kumpa vitu vya msingi kwani bado yupo ndani ya mkataba.
“Wala tusitumie nguvu kubwa katika jambo hili tusubiri hadi siku ya mwisho ya mkataba wa mchezaji kila kitu kitafahamika kama ilivyo kawaida yetu kutoa taarifa sahihi kwenye mitandao yetu ya kijamii au kiongozi husika,” alisema Mangungu.