Ajali ilivyowaua mama, watoto wanne



Bukoba. Watu wanane, wakiwemo watano wa familia moja wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha magari mawili kugongana uso kwa uso katika barabara kuu ya kutoka Lusahunga kuelekea Nyakahura wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera umebaini chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori lililokuwa linatoka Rwanda kwenda jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa juzi na Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, William Mwampaghale ilisema gari hilo aina ya Marcedes Benz lililokuwa na trela, lilikuwa likiendeshwa na Vincent Gakuba, raia wa Rwanda.

Mwampaghale alisema gari hilo liliacha njia na kwenda kuligonga gari lingine aina ya Toyota Succeed iliyokuwa inaendeshwa na mkazi wa Lusahunga, Nyamwenda Bisalo (35) na kusababisha vifo vya watu hao.


“Gari hilo tajwa (lori) liligongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Succeed na kusababisha vifo vya watu wanane ambao ni dereva wa gari dogo na abiria wake saba, kati yao watano walikuwa wa familia moja,” alisema Mwampaghale.

Kamanda huyo aliwataja wanafamilia waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo kuwa ni Mama wa familia hiyo, mkazi wa Nyamalagala mkoani Kagera, Jesca Ntahimula (45) na watoto wake wanne -- Magreth Kimuna (14), Adidas Sekanabo (12), Zabloni Sekanabo (6) na Vedastina Sekanabo (8).

Aliwataja marehemu wengine kuwa kuwa ni wakazi wa Kakona, Nyawenda Bisalo (35), Majaliwa Maige (32) na Michael Charles (28).


“Ajali ilitokea kwa sababu ya uzembe dereva wa Benz aliyehama kutoka upande wa kushoto wa barabara kwenda upande wa kulia, kitendo kilichosababisha kugongana uso kwa uso,” alisema Mwampaghale.

Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Nyakanazi.

Ajali hiyo imetokea ikiwa ni siku chache baada ya Julai 5, watu watano kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya lori la mizigo lililobeba shehena ya mahindi kufeli breki na kugonga basi dogo la abiria aina ya Coaster lililokuwa likitoka mjini Mbeya kwenda Mbarali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei alisema ajali hiyo ilitokea kwenye mteremko mkali wa barabara kuu ya Mbeya-Dar es Salaam.


Lori hilo liligonga Coaster na kuliburuza mpaka kwenye vibanda vilivyopo pembezoni mwa barabara na kusababisha vifo hivyo na majeruhi.

Ajali hiyo ilitanguliwa na nyingine ya Julai mosi, ambayo ilia ikliteketeza maisha ya watu watano na wengine 17 kujeruhiwa a katika kijiji cha Mabangwe wilayani Sikonge mkoani Tabora.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao alisema basi hilo la Sasebosa lililokuwa likitoka mkoani Mbeya kwenda Tabora.

Mbali na ajali hizo, Juni nayo haikuwa salama ambapo Juni 10, watu 20 walifariki dunia kwenye ajali ya Coaster lililogongana na lori karibu na eneo la Changarawe, Mafinga mkoani Iringa.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi alisema chanzo cha ajali hiyo kilikuwa uzembe wa dereva wa gari hiyo iliyokuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Mbeya.

Ajali nyingine ilitokea Juni 11 wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga na kusababisha vifo vya watu watano na wengine tisa kujeruhiwa baada ya Coaster waliyokuwa wamepanda kuacha njia na kupinduka.

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kalisti Lazaro alisema ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Mbaramo Tarafa ya Umba wilayani humo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad