STAA aliyetingisha kwenye usajili wa Yanga, Stephane Aziz Ki kutoka Burkina Faso yupo mtegoni akiwa na kazi ya kupindua meza dhidi ya ufalme wa Mkongomani Fiston Mayele aliyesajiliwa msimu uliopita na kufanya makubwa kwa kutupia mipira nyavuni huku akiwakuna mashabiki.
Ipo hivi. Msimu uliokwisha Mayele ndiye alikuwa kinara wa mabao 16 Yanga na mfungaji namba mbili wa Ligi Kuu Bara nyuma ya Goerge Mpole wa Geita Gold aliyemaliza na mabao 17.
Ukiachana na hilo alionyesha umahili mkubwa wa kufunga mabao makali, huku alilofunga na Biashara United, Uwanja wa Benjamin Mkapa ndilo lilikuwa bao bora la msimu.
Licha ya ufalme ndani ya Yanga, umaarufu wake ulizidi kuwa mkubwa kutokana na staili yake ya ushangiliaji ambayo ilitumika makanisani, misikitini, timu pinzani, bungeni na kwingineko.
Sasa ujio wa Aziz Ki ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili Yanga na alikotoka ASEC Mimosas alifunga mabao matatu kwenye ligi na manne Kombe la Shirikisho, huku timu yake ya taifa akiitwa kwa mara ya kwanza na kucheza mechi moja kafunga bao moja.
Jina la Aziz Ki limekuwa kubwa kabla ya kuanza kwa majukumu na ndiye habari ya mjini kwa sasa, kwani awali ilisemekana Simba nayo ilikuwa inafukuzia saini yake, lakini iliwahiwa na Yanga.
Umarufu wa Aziz Ki ni deni linalosubiriwa kulipwa uwanjani, kuhakikisha mashabiki wake wanafurahia huduma atakayotoa, kama alivyofanya mtangulizi wake Mayele kuwaaminisha kwa vitendo ufundi wake wa kucheka na nyavu.
Mbali na mastaa hao wawili, yupo winga Bernald Morrison aliyetokea Simba ni mchezaji mzuri uwanjani pia ana matukio mengi yanayoweza kumfanya akawa maarufu nje na hapo ni mbunifu wa staili ya kushangilia.
Kwa upande wa Simba msimu uliopita hakukuwa na mchezaji aliyejiwekea ufalme wake nafasi ambayo ipo wazi kwa ligi inayoanza Agosti 17 anayefanya vizuri ndiye atakayewateka mashabiki.
Kutokana na umarufu wa mastaa hao, beki wa zamani wa timu hiyo, Bakari Malima alisema ni kama mtihani kwao utakaojibiwa kwa matendo uwanjani msimu ujao.
“Mayele tayari uwezo wake unajulikana, kazi itakuwepo kwa Aziz Ki kuonyesha wanachokitarajia mashabiki wake, naamini akikichukulia kwa upana mkubwa atatunza thamani yake,” alisema.
Hoja yake ilungwa mkono na straika wa zamani wa timu hiyo, Said Bahanuzi aliyesema “Umarufu wa mchezaji asipofanya vizuri unaweza ukageuka maumivu, hivyo kujulikana kabla ya kucheza ni kama deni kwake msimu utakapoanza kuonyesha makali yake,” alisema.