Dar es Salaam. Kuna sintofahamu imeibuka kuhusu sarafu ya Sh500 baada ya kuonekana baadhi zenye alama tofauti kwenye mzunguko.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi zimeeleza kuwa sarafu hizo zenye baadhi ya alama tofauti zipo kwenye mzunguko na zinatumika kufanya manunuzi mbalimbali hususan jijini Dar es Salaam.
Katika uchunguzi wake Mwananchi limeshuhudia baadhi ya sarafu hizo katika mazingira tofauti.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilipoulizwa na Mwananchi imesema inaendelea na uchunguzi wa suala hilo.
Kwa mujibu wa Sheria ya BOT ya mwaka 2006, mamlaka pekee ya kutengeneza, kutoa fedha, kubuni na kuagiza (noti na sarafu) kwa uhalali wa malipo na kukidhi mahitaji.
Julai 11, mwaka huu maofisa wa BoT waliokuwa kwenye maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa Jijini Dar es Salaam walipoulizwa na kuonyeshwa moja ya sarafu hizo, walimtaka mwandishi wa gazeti awasiliane na wizara kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, alipoulizwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alishauri suala hilo lipelekwe Idara ya Sarafu ya BoT huku akitoa onyo vya vitendo vyovyote vinavyohusiana na kuchapisha na kusambaza noti au sarafu.
Idara ya fedha ya BoT ililitaka gazeti hili liandike barua kwa Ofisi ya Gavana wa BoT kuomba ufafanuzi kupitia watalaamu wa idara hiyo.
Baada ya kuandika barua hiyo Julai 14 na Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florens Luoga amethibitisha kuipokea na kuwa tayari wameanza uchunguzi.
“Tumepokea barua yenu, suala hili tunalifanyia kazi,” alijibu Profesa Luoga Julai 21.
Tofauti za muonekano
Sarafu hiyo inaonekana kuwa tofauti na Sh500 zilizoingizwa kwenye mzunguko na BoT Oktoba 2014 katika baadhi ya alama.
Akizungumza na Mwananchi, George Migoba mtoza ushuru katika moja ya huduma za choo jijini Dar es Salaam, alidai karibu kila siku hupokea sarafu kama hiyo na kuwarudishia wanaozitoa ili wambadilishie.
“Hii sarafu niliigundua miezi minne iliyopita, makondakta wengi wakija nazo hapa nawarudishia, au mteja anayetaka huduma...ukiitazama wamekosea kuikata, halafu ni nyepesi, madini yake yako kama bati hivi,” alidai Migoba.
Jasmin Peter, mtoa mkata tiketi katika Kituo cha Mwendokasi Manzese pia alisema amewahi kupokea sarafu za namna hiyo mara kadhaa.
“Napokea mara kwa mara, lakini nikawa na wasiwasi, najiuliza lini Serikali imetoa sarafu nyingine? nilishtuka,” alisema Jasmin.
Baadhi ya abiria wanaosafiri kwa daladala walipozungumza na Mwananchi walikiri ugumu wa kuitambua sarafu hiyo hivyo baadhi yao wakiitaka Serikali kuchukua hatua za haraka ili kuondoa utata huo.
Rashid Kassim, muuza sarafu kwenye moja ya vituo vya daladala alisema “kama ni feki imeshasambaa mno, mie ninauza chenji za Sh40,000 kwa makondakta na wala hakuna anayeshtuka, sasa huko ninakozichukua itakuwaje?” alihoji Kassim.
Baadhi ya makondakta pia walithibitisha kupokea sarafu hiyo mara kadhaa huku wengine wakiirejesha kama chenji kwa abiria ili kukwepa hasara.
Kondakta wa daladala inayofanya safari zake kati ya Tabata Kinyerezi na Mnazi mmoja, Boazidi Adam alisema “siwezi kumaliza mwezi bila kukutana na sarafu hii, nilianza kuipokea mwanzoni mwa mwaka huu, wakati mwingine naitambua kwa hisia ya sauti mlio,” alisema Adam.
“Kwa mfano mimi huwa nakusanya Sh500 za thamani ya Sh25,000 au zaidi kila siku, na si rahisi kuzikagua zote,” alisema kondakta huyo.
Kwa upande wake Mickdadi Abdallah, dereva wa daladala ya Masaki-Simu 2000, alishauri mamlaka husika ichukue hatua na kutoa taarifa kuondoa mkanganyiko.
Utofauti wake
Baadhi ya alama zinazotajwa kuwa ni tofauti ni sarafu moja kuonekana inag’aa zaidi na nyingine imefifia, nyepesi na hata mlio wake ni tofauti ikiangushwa sakafuni.
Aidha, kwenye sura ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume taswira ya nyati nako kumeonekana utofauti.
Kosa la kughushi, utakatishaji
Pamoja na kuelekeza suala hilo lifuatiliwa BoT, Tutuba alitoa onyo kwa yeyote anayejihusisha na utengenezaji na usambazaji wa sarafu.
“Kusambaza na kutengeneza sarafu adhabu yake ni kifungo, chini ya makosa ya kugushi nyaraka za Serikali, pili kuna anayeweza kushtakiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha, sheria ipo ya makosa ya uhujumu uchumi kwani atafilisiwa mali zake na kushtakiwa,” anasema Tutuba na kuongeza:
“Kwa sababu kusambaza fedha feki inaweza kusababisha mgogoro katika uchumi, kwa hiyo niwasisitize Watanzania wote pale unapoona sarafu feki toa taarifa BoT au polisi, kwa wanaotengeneza waache mara moja.”
Tishio la kiuchumi
Wakati wasiwasi ukiendelea kuhusu sarafu hiyo, wachumi wameeleza hatari kuingia fedha haramu kwenye mzunguko ukiwemo mfumuko wa bei.
Dk Donald Mmari, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Repoa anasema: “Ni hatari pesa feki zikiingia kwenye mzunguko, kwanza kabisa monitory policy (sera ya fedha ya BoT) haiwezi kufanya kazi kwani itakuwa inadanganywa na pesa iliyoongezeka mtaani,” alisema.
“Kwa mfano Serikali inapoingiza Sh1 trilioni kwenye mzunguko kumbe tayari kuna Sh1.5 trilioni, hiyo inasababisha hata bidhaa kupanda bei na utakatishaji wa fedha pia. Kwa hiyo Serikali ifanye bidii kuondoa kwenye mzunguko sarafu hiyo na iwatafute na kuwachukulia hatua,” alisema Dk Mmari.
Sifa za sarafu
Kwa mujibu wa BoT umbo la sarafu ya Sh500 ni la duara lenye michirizi pembezoni, kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5.
Ina rangi ya fedha na imetengenezwa kwa madini aina ya chuma (Steel) na “Nickel”
Kwa mbele ina sura ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa mbugani.
Ina alama maalum ya usalama iitwayo “latent image” iliyopo upande wa nyuma ambayo ni kivuli kilichojificha. Kivuli hiki huonesha thamani ya sarafu ‘500’ au neno ‘BOT’ inapogeuzwa-geuzwa.