Breaking: Kina Mdee waibwaga Chadema mahakamani



WABUNGE Viti Maalum 19 wakiongozwa na Halima Mdee, wamekibwaga Chama cha Chadema mahakamani baada ya Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, kukubali ombi lao la kufungua kesi ya kupinga mchakato uliotumiwa na chama hicho kuwavua uanachama. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa tarehe 8 Julai, 2022, na Jaji Mustafa Ismail, kuhusu maombi hayo yaliyofunguliwa na kina mdee dhidi ya Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Jaji Ismail amewataka kina Mdee wafungue kesi hiyo ndani ya siku 14 kuanzia leo.

Katika maombi hayo, Mdee na wenzake 18 waliiomba mahakama ifanye mapitio ya kimahakama dhidi ya mchakato ambao Chadema ulitumia kuwavua uanachama, wakidai haukuwa halali kwani haukufuata sheria kwa kuwa hawakupewa nafasi ya kusikilizwa na kugubikwa na upendeleo.


Hata hivyo, Chadema kupitia mawakili wake, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, waliiomba mahakama ikatae ombi la kina Mdee kwa kuwa hoja zao hazina mashiko wakidai walipewa nafasi ya kusikilizwa.


Wakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala (katikati) wakiwa mahakamani
Mbali na Mdee, baadhi ya wabunge wengine ni Jesca Kishoa, Ester bulaya, Esther Matiko, Hawa Mwaifunga, Grace Tendega, Angesta Lambart, Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Wabunge hao walivuliwa uanachama wa Chadema tarehe 27 Novemba 2020, siku tatu baada ya kuapishwa na Spika Job Ndugai, kuwa wabunge viti maalumu kupitia chama hicho.


Mdee na wenzake walituhumiwa kwa makosa ya kusaliti msimamo wa Chadema wa kutopeleka wawakilishi wake bungeni, wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, kwa madai kwamba haukuwa huru na wa haki.




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad