CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo Jumapili kimemtaka Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ajiuzulu nafasi hiyo kwa kushindwa kuwatimua bungeni wabunge 19 Chadema waliovuliwa uanachama na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kubariki uamuzi huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Pia kimeitaka CCM kupitia Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu Mwenyekiti Bara, Abdulrahman Kinana na Katibu wake, Daniel Chongolo kuhimiza viongozi wake walio katika serikali kuilinda na kuiheshimu Katiba ya nchi kwani ndio chama kinachoshika hatamu ya uongozi.
Hatua hiyo imekuja baada ya tarehe 22 Juni, mwaka huu Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam ilitupilia mbali shtaka la zuio kutoka kwa wabunge 19 wa viti maalumu wa Chadema kupinga kufukuzwa uanachama wa Chadema.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 26 Juni, 2022 jijini Dar es Salaam, Spika wa bunge la wananchi Chadema, Celestine Simba amesema chama hicho kinashangazwa na ukimya wa Spika Tulia licha ya mahakama kutoa huku dhidi ya wabunge hao 19.
Amesema Chadema tayari kimepokea nakala ya hukumu na kimewasilisha hukumu hiyo na barua kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Bunge ili kusisitiza kufukuzwa kwa wabunge na wasaliti hao.
“Spika Tulia anao wajibu wa kuilinda na kuihifadhi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa aliapa kufanya hivyo wakati anakula kiapo cha kukishika nafasi ya kuwa Spika wa Bunge.
“Kuendelea kubaki na wabunge hao bungeni, ni ishara tosha kwamba yeye Spika pamoja na Serikali chini ya CCM ni watu ambao hawapaswi kuaminika kwa kuwa hawaamini katika makubaliano yoyote,” amesema.
Aidha, amesema licha ya vyombo vya habari kuandika kuwa wabunge hao wamerejesha kesi mahakama, lakini mpaka sasa hakuna zuio lolote lililotolewa na mahakama kwamba kesi imefunguliwa wala ‘summons’ kwa upande wowote kuitwa mahakamani.
Kutokana na hali hiyo amesema Chadema inaendelea kusisitiza Dk. Tulia aheshimu Katiba ya nchi kwa kutekeleza jukumu hili la kuwafukuza wabunge wasio na chama bungeni bila kujali urafiki wao.
“Kuendelea kumuacha Spika kufanya anavyotaka juu ya chombo hiki muhimu cha kutunga sheria, ni ishara tosha kwamba hata hizo sheria zinazotungwa hazina maana yoyote kwa kuwa sio lazima kuzifuata,” Spika wa bunge la wananchi.
“Hakuna maana yoyote kwa msomi wa sheria kuongoza muhimili unaotunga sheria lakini yeye ndio kiongozi wa kuvunja sheria hizo.
“Kama ilivyokuwa kwa Ndugai, Dk. Tulia naye aondolewe kwa kuwa hatoshi, hawezi kuilinda, kuiheshimu wala kuuheshimisha muhimili wa Bunge anaouongoza. Nchi yetu ni nchi inayopaswa kuongozwa kwa kufuata sheria na katiba.
“Ameshindwa kusimama katika nafasi yake kufanya maamuzi yanayokinzana na urafiki wake kwa hiyo anapata kigugumizi, kwa sababu hiyo sisi Bunge la Wananachi tunamtaka aachie nafasi hiyo kwa kuwa hatoshi,” amesema
Amesema hali hiyo inaidhalilisha nchi, katiba ya nchi pamoja na chama chake cha CCM ambacho kimempa ridhaa ya nafasi aliyo nayo sasa.
Amesema mara ya kwanza Spika Tulia alisema hawezi kuwaondoa bungeni kwa sababu wabunge hao wamefungua kesi mahakama ilihali wakati anatoa tamko hilo, hapakuwa na zuio lolote la mahakama.
“Mpaka muda huu hakuna summons wala taarifa yoyote ya mahakama kuhusiana na kufunguliwa kwa kesi wala kuwekwa kwa zuio lolote, tunajiuliuza Dk. Tulia kuendelea kwa wabunge hao haramu kufuja fedha za umma ni nini kilicho nyuma mpaka kuendelea kuwatunza wabunge hao haramu,” amehoji.
Wabunge hao wanaotakiwa kutimuliwa bungeni ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnes Lambart, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa na Hawa Mwaifunga.
Wengine ni Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.
Tarehe 12 Mei, mwaka huu Baraza Kuu la Chadema liliunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho wa kuwafukuza uanachama wabunge 19 wa viti maalum akiwamo aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake (BAWACHA), Halima Mdee.