Chadema yazuia 11 kuendelea na uongozi




Mbeya. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amewazuia wajumbe 11 wa kamati tendaji ya Mkoa wa Mbeya waliokata rufaa baada ya kuondolewa kwenye uongozi, kutojihusisha na shughuli zozote za uongozi hadi rufaa zao ziamuliwe.

Mnyika alitoa uamuzi huo juzi jijini Mbeya alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatima ya viongozi hao.

Alisema tayari amepokea nakala ya rufaa zao ofisini kwake na ameiagiza ngazi inayohusika ianze kushughulikia rufaa hizo.

Alisema wakati rufaa yao zinashughulikia, wana haki ya kushiriki shughuli zote za chama kama wanachama wa kawaida na si viongozi, huku akiweka bayana kwa kuwa hawajafukuzwa uanachama.


 
“Nimepokea nakala yao, kifungu pekee kilichopo kwenye kanuni za chama ngazi ya chini ikifanya uamuzi inatakiwa kuwasilisha kwenye ngazi ya juu uamuzi waliofanya ndani ya siku 14,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema kwa sasa msimamo wa chama ni kuwataka wale wote walio ondolewa na uongozi wa Kanda kutoendelea kujihusisha na shughuli kama viongozi mpaka hapo taarifa ya kamati kuu itakapotoa taarifa za mapitio ya rufaa zao.

Alisema taratibu za chama zinatoa muda wa kukata rufaa wa kikatiba ambao uko pia kwenye mikoa mingine na si Mbeya pekee, hivyo maelekezo ya chama ni kutaka viongozi hao wasubiri majibu ya rufaa.

Kwa upande mwingine, Mnyika alisema licha ya kuwepo katika kipindi cha mpito cha kuhitaji Katiba mpya amewataka viongozi wa chama kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga kwa mfumo wa kieletroniki ili kupata fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija maarufu ‘mzee wa upako’ alisema uamuzi wa Mnyika ni sahihi na atabaki kama mwanachama na kutojihusisha na shughuli kama kiongozi.

“Nimemsikia Katibu Mkuu yuko sahihi kabisa kwa sasa tutaendelea kukipigania chama kama wanachama na si viongozi mimi na wenzangu 11 tulioondolewa na uongozi wa Kanda kwani sisi bado ni wanachama hai wa Chadema,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad