Shakira anaweza kufungwa jela miaka minane na faini ya zaidi ya euro milioni 23 iwapo atapatikana na hatia katika kesi ya ulaghai wa kodi.
Mwimbaji huyo wa Colombia anashutumiwa kwa kushindwa kulipa ushuru wa €14.5m (£12m) kati ya 2012 na 2014.
Mapema wiki hii Shakira alikataa ofa ya kumaliza na kufunga kesi hiyo. Tarehe ya kesi bado haijawekwa
Taarifa kutoka kwa wawakilishi wa Shakira ilisema "ana uhakika kamili wa kutokuwa na hatia" na anaona kesi hiyo kama "ukiukaji wa haki zake".
Nyota huyo alishtakiwa kwa kukwepa kulipa ushuru mwaka wa 2018. Waendesha mashtaka walisema alikuwa akiishi Uhispania kati ya 2012 na 2014 huku akiorodhesha makazi yake rasmi mahali pengine.
Watu wanaokaa zaidi ya miezi sita nchini wanachukuliwa kuwa wakazi kulingana na kanuni ya utozaji ushuru. Lakini Shakira anasema hakuwa akiishi Uhispania wakati huo.
Hati kutoka kwa waendesha mashtaka iliyoonekana na Reuters inadai Shakira alinunua nyumba huko Barcelona mnamo 2012, ambayo ilikuja kuwa nyumba ya familia yake na mshirika wake wa wakati huo, mchezaji soka wa klabu ya Barcelona Gerard Piqué.