SIMON Msuva ameshinda kesi yake katika Shirikisho la Soka la Kimataifa dhidi ya klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, ushindi unaomfanya staa huyo Mtanzania kuwa bilionea f’lani hivi kutokana na mkwanja mrefu ambao Fifa imeiamuru klabu hiyo imlipe.
Mshambuliaji huyo ambaye yupo nje ya uwanja kwa takribani miezi saba tangu azinguane na klabu hiyo, ameshinda kesi yake dhidi ya Wydad aliyoifungua Novemba mwaka jana ambapo hukumu imeamuru alipwe dola za kimarekani 700,000 ambazo ni zaidi ya Sh 1.6 bilioni za Kitanzania.
Hukumu hiyo ya Fifa ilitolewa Julai 11 na Wydad imetakiwa iwe imeshampa fedha hizo ndani ya siku 15, yaani Msuva amesaliwa na siku chache tu kabla ya kuwa bilionea kwa fedha hizo atakazolipwa.
Msuva alisaini mkataba wa miaka minne na timu hiyo, lakini alilazimika kuukatisha mwishoni mwa mwaka jana kutokana na kuidai klabu hiyo malimbikizo ya mshahara na pesa za usajili.
Sasa unaambiwa kwa fedha hizo Sh 1.6 bilioni, Msuva ana uwezo wa kutisha sana kwa aina yoyote ya matumizi atakayoamua kuyafanya.
Mwanaspoti inakuletea kufuru ya fedha hizo ambayo Msuva akiamua anaweza kufanya.
KUZITUMIA MIAKA 87
Unaambiwa kama Msuva ataamua kutumia kila siku Sh 50,000 (bila ya kuzidisha au kupunguza hata senti) katika mihela hiyo basi itamchukua muda wa miaka 87 kuzimaliza.
Yaani atazitumia hadi awe kikongwe wa miaka 115 (ukijumlisha na umri wake wa sasa wa miaka 28) Mungu akimjaalia umri mrefu.
BODABODA 800
Kama Msuva ataamua kutaka kununua bodaboda ili ziwe zinamuingizia fedha kila uchao, basi akienda dukani na fedha hizo anapata pikipiki 800 za bei ya Sh 2 milioni kila moja.
Yaani kwa jiji la Dar es Salaam, jamaa atakuwa na bodaboda ambazo zitatapakaa kila kona na kumkusanyia fedha za kutosha akiamua kuifanya biashara hiyo. Bodaboda 800 sio mchezo!
BAJAJ ZAIDI YA 200
Kama mwamba huyo ataamua kujinunulia zake Bajaj ambazo zinauzwa Sh 8 milioni, basi Msuva atamiliki zaidi ya Bajaj 200 na kama ataziweka chata zake, basi itakuwa balaa kwa jijini la Dar es Salaam kwa namna huduma hiyo ilivyo kimbilio la wakazi wengi wa jiji hilo.
KUMILIKI KIJIJI
Kama haitoshi Msuva akiamua kuwekeza fedha zake kwenye kumiliki nyumba, akiamua kwenda eneo la Mbagala na kununua kila nyumba kwa Sh 50 milioni, basi anaweza kuwa na kijiji kizima kitakachopewa jina lake kwani atakomba nyumba zisizopungua 32.
Iwapo ataamua kutua Tandale au Mwananyamala kama sio Kigogo na Mburahati ataweza kupata nyumba kwa bei ya Sh 30 milioni basi atapata nyumba 53. Hapo kwanini Msuva asiwe na mtaa wake kabisa?
NOAH/ IST ZA KUTOSHA
Kiungo mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania kama ataamua kuwekeza fedha zake kwenye magari na kuamua kutinga yadi za kuuzia vyombo hivyo vya moto na kuchagua kati ya Toyota Noah au Toyota IST ambazo huuzwa kwa wastani wa bei ya Sh 15 milioni basi jamaa atajibebea zake magari 106.
Yaani akiamua kufungua kampuni ya kusafirisha watu kama ilivyo Uber au Bolt basi jamaa atakimbiza sana na gari zenye chata zake, ambapo wateja watakuwa wakiziita popote walipo na kupata huduma