Mwanza. KLABU ya Geita Gold imethibitisha kuwa imeruhusiwa kufanya usajili na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) baada ya kukidhi vigezo kwa kumalizana na kocha Etienne Ndayiragije aliyekuwa anaidai.
Juni 25, mwaka huu FIFA iliifungia timu hiyo kusajili hadi itakapomlipa aliyekuwa Kocha wake, Ettiene Ndayiragije ambaye alifungua madai akidai fidia ya kuvunjiwa mkataba na malipo mengine wakati akiifundisha timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo ambayo imetolewa leo Julai 13 na Mtendaji Mkuu, Simon Shija timu hiyo imemalizana na adhabu ya FIFA ya kuzuiwa kufanya usajili.
Shija amesema klabu yao imetekeleza matakwa yote ya kisheria na kikanuni kwa kuzingatia miongozo ya shirikisho hilo na sasa ipo huru kuendelea na utendaji wake.
"Uongozi wa klabu ya Geita Gold unapenda kuwataarifu mashabiki, wadau na wapenda michezo kuwa imemalizana na adhabu ya FIFA iliyokuwa na zuio la kuifungia kufanya usajili,"
"Tunaomba wadau kuendelea kushirikiana na klabu na milango ya udhamini ipo wazi, klabu imepanga kufanya vizuri msimu ujao ili kuendeleza hali ya ushindani katika michuano ya ndani na kimataifa," amesema Shija.
Kabla ya taarifa hiyo, Geita Gold ilikuwa haijaanza kufanya usajili wala kutambulisha mchezaji yeyote kuelekea msimu mpya huku kukiwa na ukimya mkubwa, lakini baada ya taarifa hiyo vigogo hao wameanza mikwara wakitajwa kumalizana na Ramadhan Chombo na baadhi ya nyota wengine.