UNAWEZA kusema moshi mweusi umezingira katika klabu ya Yanga baada ya msemaji wake maarufu, Haji Manara kufungiwa kujihusisha na soka ndani na nje ya Tanzania kwa muda wa miaka miwili, lakini akitakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 20.
Manara alikutwa na hatia katika shauri lililowasilishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na sekretarieti ya shirikisho hilo kutokana na vitendo vya ukiukaji wa maadili.
Msemaji huo alidaiwa kumtolea kauli ya vitisho, Rais wa TFF, Wallace Karia katika eneo la VVIP siku ya mechi ya fainali ya Kombe la FA iliyochezwa Julai 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana baada ya hukumu hiyo kutangazwa, Manara alisema hajafanya uamuzi wowote kama atakata rufani au ataitumikia adhabu hiyo kama ilivyotolewa na Kamati ya Maadili.
Hata hivyo, Manara alisema bado hajapokea rasmi nakala ya hukumu ya kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Wakili Mwita Waissaka.
"Sidhani," Manara aliliambia gazeti hili kwa kifupi.
Msemaji huyo wa zamani wa Simba aliendelea kusema anamshukuru Mungu kwa kila jambo.
"Iwe ni jambo la kheri au shari, neno langu kuu ni kumshukuru muumba mbingu na ardhi kwa neno moja kubwa na lenye maana pana sana.
Alhamdulillah," Manara alisema.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said alipotafutwa na gazeti hili jana jioni kuzungumzia hukumu iliyompata Manara, hakupatikana.
Katibu wa Kamati ya Maadili, Walter Lungu alisema kamati hiyo ilijiridhisha na utetezi wa Manara na kumpa hukumu ya kutojihusisha na masuala ya mpira wa miguu pamoja na faini kwa kufuata Kanuni ya Katiba ya TFF kifungu cha 73 (5) na 73 (6).
Lungu alisema kulingana na Katiba na kifungo cha kanuni hiyo ya TFF adhabu hiyo itaanza kutumika rasmi kuanzia jana.
“Baada ya Kamati kujiridhisha kwa ushahidi mlalamikaji na utetezi wa mlalamikiwa, Manara anahukumiwa na matendo hayo baada ya kuitwa mara kadhaa na kukubali kutoa kauli hiyo.”
“Julai 11, mwaka huu, kamati ilikutana kwa mara ya kwanza baada ya shauri hilo kuletwa mezani kwetu kwa kuhoji pande zote mbili, kwa upande wa mlalamikaji alileta ushahidi kwa maneno aliyoyasema Manara; “Wewe unanifuatafuata sana, hii ni mara ya tatu, sikuogopi kwa lolote, kwa chochote na huwezi kunifanya chochote, nina uwezo wa kukufanya chochote na huna cha kunifanya,” akiwa katika jukwaa la VVIP kwenye mchezo huo,” alisema Lungu.
Aliongeza baada ya kuondolewa katika jukwaa kuu alipokwenda kumfanyia taharuki, baada ya mpira kumalizika Manara alimfuata Katibu wa TFF, Wilfred Kidao akiwa na pakti ya boksi ya sigara na kibiriti cha gesi na kurudia maneno hayo hayo.
“Mlalamikiwa alikiri kufanya makosa hayo na aliomba msamaha kwa mlalamikaji lakini kwa wadau wa soka, ila kulingana na kanuni za Katiba ya TFF, Manara atatumikia adhabu hiyo kuanzia sasa,” alisema Lungu.
Naye mwenyekiti wa kamati hiyo, Wakili Waissaka alisema Manara anaruhusiwa kukata rufani kama hakuridhika na uamuzi wa kamati yake.
Waissaka alisema kwa hukumu hiyo, Manara hataruhusiwa kushiriki kwa sababu Yanga ni mwanachama wa TFF, hivyo wanatakiwa kufuata maelekezo yasiyoendana kinyume na shirikisho hilo.