Rais wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa amewasilisha barua ya kujiuzulu leo muda mfupi baada ya kuwasili nchini Singapore siku moja baada ya kuikimbia nchi yake kufuatia shinikizo la maandamano ya umma.
Duru kutoka Serikali mjini Colombo zinasema Kiongozi huyo ametuma barua ya kujiuzulu kwa njia ya baruapepe kwenda kwa Spika wa Bunge la Sri Lanka lakini haikufahamika mara moja iwapo njia aliyotumia inaruhusiwa kisheria.
Rajapaksa, Mkewe na Walinzi wawili waliwasili leo mchana katika uwanja wa ndege wa Changi mjini Singapore City wakitokea visiwa vya Maldives ambako Kiongozi huyo alikwenda baada ya kuitoroka Sri Lanka jana Jumatano.
Nchini Sri Lanka kwenyewe vikosi vya jeshi vimetawanywa kwenye Mji Mkuu Colombo na maafisa wa usalama wameweka vizuizi vikali nje ya majengo ya Bunge kufuatia wasiwasi kwamba waandamanaji wangejaribu kuyavamia.