Hoja tatu za kesi mpya kina Mdee



HATIMAYE Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee na wenzake 18 wamefungua shauri katika Mahakama Kuu Masjala Kuu kupinga kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiomba amri tatu zitolewe.

Halima Mdee.
Mdee na wenzake walifungua shauri hilo jana, likisajiliwa kwa namba 36/2022, wakiiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama na kisha itoe amri tatu.

Katika shauri hilo, wabunge hao wanaiomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama na pia iwalazimishe CHADEMA kuwapa haki ya kuwasikiliza.

Pia wanaomba kuwekwe zuio dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua hatua yoyote hadi malalamiko yao yatakapotolewa uamuzi.

Pamoja na mambo mengine, wabunge hao wanadai kuwa mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama haukuzingatia matakwa ya kisheria na misingi ya haki - kwamba hawakupewa haki ya kusikilizwa.


 
Katika kiapo cha Mdee, anadai kuwa Novemba 25, 2020, CHADEMA walimtumia barua ya maelezo ya makosa yake kupitia mtandao wa WhatsApp na kumtaka ahudhurie kikao cha Kamati Kuu kilichopangwa kufanyika Novemba 27, 2020, ikiwa ni taarifa ya siku mbili tu.

"Kutokana na hasira na vitisho vya usalama na kauli za Katibu Mkuu wa CHADEMA kwa umma kuwa ni wasaliti, matokeo yake wanachama wa chama hicho walianza kutoa vitisho kwa kiwango cha kushutumiwa na hata kuitwa Covid- 19," Mdee anadai katika kiapo chake.

Mdee pia anadai kuwa kutokana na hayo, aliingiwa na hofu ya kushambuliwa na wanachama wa CHADEMA waliochochewa na kauli za viongozi wa chama hicho, akiwamo Katibu Mkuu, John Mnyika.

Anadai kuwa kutokana na hofu hiyo, kwa kuzingatia kuwa siku ya kupata wito wa kufika mbele ya Kamati Kuu, Dar es Salaam Novemba 27, 2020, akiwa jijini Dodoma, aliiandikia Kamati Kuu akiomba ahirisho la kikao hicho na kuongezwa muda.

Mdee anadai lengo lilikuwa ni kufanya hali ipoe na kujihakikishia usalama na pia kupata muda wa kutosha kujiandaa kwa usikilizwaji na kuwasilisha utetezi wake.

Anadai kuwa kutokana na nia ovu, ombi lake lilikataliwa na Kamati Kuu kupitia barua aliyotumiwa na Katibu Mkuu kupitia WhatsApp Novemba 26, 2020, hivyo shauri lake likasikilizwa na kuamuliwa upande mmoja.

"Nilikata rufani Baraza Kuu Desemba 23, 2020 nikipinga uamuzi huu wa Kamati Kuu na utaratibu wote uliotumika kwa kuwa sikupewa haki ya kusikilizwa na hivyo kukiukwa kwa haki yangu ya msingi," Mdee anadai katika hati hiyo.


 
Anadai sababu iliyotolewa na Baraza Kuu kumfukuza uanachama ilitokana na makosa yasiyo na maana na yasiyothibitika kuwa alikula njama kujiteua mwenyewe na kuapa kuwa mbunge wa viti maalum.

Mdee anadai kwamba mara tu baada ya kula kiapo Novemba 24, 2020, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Mnyika, alimtaja yeye na wenzake 18 kama wasaliti.

Anadai kuwa Mnyika alikwenda mbali alipowaalika wanachama wa CHADEMA na umma kwa kutoa mapendekezo kuhusu vikwazo vinavyofaa kuwawekea, hata kabla hajapewa barua au maelezo ya makosa yake na nafasi ya kusikilizwa na Kamati Kuu.

Uamuzi huo wa Baraza Kuu ulitokana na rufani walizozikata Mdee na wenzake kupinga uamuzi wa awali wa kuwavua uanachama uliotolewa na Kamati Kuu Novemba 27, 2020, iliyowatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila ridhaa ya chama.


Katika shauri hilo, Mdee na wenzake wanawakilishwa na Mawakili Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad