Staa wa Bongo Ibrahim Abdallah Nampunga almaarufu Ibraah ameweka wazi kuwa ameridhika na label yake ya Konde Music Worldwide.
Akizungumza na waandishi wa habari wikendi, Ibraah alikiri kuwa ameridhika na jinsi anavyosimamiwa katika lebo hiyo ya Harmonize.
Hata hivyo alibainisha kuwa hatasita kuondoka Konde Gang endapo ukiukwaji wa mkataba utawahi kutokea.
"Kila biashara ina mipaka. Mimi nimesaini na Kondegang watangaze biashara yangu, wapromoti muziki wangu na nyimbo kali wazifanyie haki, kama wimbo ni wa bei fulani basi uwe ya bei hiyo. Hivyo ndo ambavyo naishi, lakini ikiwa tofauti nitawafuata nitawaambia kwa sababu wao ndo wakubwa wangu," Ibraah alisema
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 23 aliisifia sana lebo yake kwa kumkuza hadi kuwa mwanamuziki tajika.
Ibraah pia alikiri kwamba bado anamtegemea Harmonize kupromoti muziki wake licha ya kuwa tayari amejizolea umaarufu mkubwa.
"Yeye ni ndugu yangu na amenitoa mbali. Ukimzungumzia Harmonize ni sawa na kuzungumzia kitovu cha Ibraah. Bila Harmonize watu wengi wasingemjua Ibraah," Alisema.
Katika kipindi cha takriban wiki mbili ambacho kimepita kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu mikataba ya wasanii katika lebo tofauti za Bongo.
Wiki jana mtayarishaji wa muziki P-Funk majani alishtumu lebo ya Diamond, WCB kwa kuwakandamiza wasanii wake.
"Kitu kimoja nachopenda uwe mtu wa haki, usifanye biashara kuangamiza wenzio. Wale wanamdidimiza msanii yule wanachukua asilimia kubwa alafu yeye anabaki na ndogo. Akienda kuimba anatumbuiza bado anakatwa hela kubwa aiiuza kwenye album anakatwa hela kubwa," P-Funk alisema katika mahojiano, maneno ambayo alielekeza kwa WCB.
Siku chache baadae Diamond alijitokeza kuyatupilia mbali madai ya kuwakandamiza wasanii huku akibainisha kuwa mikataba ya lebo yake huwa ya haki.
Haya yalijiri siku chache baada ya Rayvanny kugura WCB baada ya kuwa chini ya usimamizi wake kwa miaka sita.
“Miaka 6 sasa tangu tumeanza kufanya kazi pamoja na hii timu yangu, familia yangu, WCB Wasafi. Upendo, umoja vimekuwa nguzo kubwa saba kama timu. Mengi nimejifunza lakini pia mengi tumefanikisha tukiwa pamoja.. Shukrani za dhati kwa familia yangu Wasafi lakini pia kwa ndugu yangu Diamond Platnumz kwa kunipa nafasi dunia ione kipaji change nilichobarikiwa na mwenyezi Mungu ili kufika hapa nilipofika, kusaidia familia yangu na kufanikisha mengi katika maisha yangu,” Rayvanny alisema kupitia kanda ya video ambayo alipakia Instagram kutangaza hatua yake kuondoka Wasafi.
Ibraah ameweka wazi kuwa yupo tayari kufanya kazi na Rayvanny baada ya yeye kuondoka lebo hiyo pinzani.
"Yeye ni ndugu yangu na anafanya vizuri kwa upande wake. Kama itatokea tutakuwa na makubaliano. Lazima ufanya colabo kwa makubaliano," Alisema katika mahojiano.