Idadi ya washtakiwa katika kesi namba 11 ya 2022 dhidi Jamhuri wanaodaiwa kufanya njama ya mauaji ya askari polisi katika pori tengefu la loliondo wilayani Ngorongoro imeongezeka kutoka washtakiwa 25 na kufikia washtakiwa 27
Wakili wa serikali Upendo Shemkole mbele ya hakimu Mkazi Arusha anaesikiliza shauri hilo Heriet Mhenga ameiambia mahakama kuwa mnamo tarehe tano mwezi wa saba mwaka huu, walileta mabadiliko katika hati ya mashtaka ya kuongeza washtakiwa wengine wawili ambao wanafikisha idadi ya washtakiwa ishirini na saba na kuiomba mahakama kumpa ridhaa ya kuwasomea tena washtakiwa hao kesi inayowakabili kwa ujumla.
Maombi hayo yamepingwa na jopo la mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na wakili Jeremia, Mtebesya ambapo wameeleza kuwa utaratibu uliotumika wa kubadilisha hati hiyo haujafuata sheria na taratibu..
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashataka mawili ambapo shtaka la kwanza linalowakabili ni kufanya mauaji ya askari polisi namba G 4200 Koplo Galus Mwita mnamo June 10 mwaka huu katika eneo la Serie Ololosokwan Pamoja na kupanga njama za mauaji kwa viongozi wa serikali waliokuwa wakifanya zoezi la uwekwaji wa mipaka katika pori tengefu la loliondo.