KAA karibu na Bernard Morrison. Huwa haishiwi maneno. Majuzi nilimsoma mahala akimwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ampatie uraia wa Tanzania ili aweze kuichezea timu ya taifa ya Tanzania.
Nadhani ameshakata tamaa ya kuichezea timu ya taifa ya Ghana. Lakini hapo hapo amedai anaipenda sana nchi ya Tanzania. Najua Morrison yupo ‘serious’ na maombi yake yamenifikirisha kwa namna mbili.
Kitu cha kwanza naendelea kuwashangaa Watanzania kwa namna ambavyo wanaona ajabu mwanamichezo akipewa uraia. Kwetu sisi Uraia ni kitu kigumu na cha ajabu. Ni kama ambavyo baadhi yetu wameendelea kumlaumu Kibu Denis kwa misingi ya kumbagua uraia wake wa kupewa.
Kibu akikosea uwanjani kuna wanaosikika “Tutakuvua uraia”. Wengine utawasikia wanasema “Huyu sijui kwa nini tulimpa uraia.” Kwetu sisi uraia ni dili kweli kweli. Hatushangai kuona kwa wenzetu ni jambo la kawaida tu.
Kuna Watanzania kibao wamepewa uraia katika nchi za watu kwa sababu tofauti. Kuna wale walioishi muda mrefu. Kuna wale ambao wana vipawa mbalimbali. Kuna wale waliopata tu bahati ya kuomba uraia na wakapewa.
Katika michezo kuna mastaa mbalimbali waliopewa uraia tena katika nchi ngumu. Kuna Wabrazil wamewahi kupewa uraia wa Japan kwa ajili ya kukiwakilisha kikosi cha timu ya taifa ya Japan. Kuna Wabrazil pia wamewahi kupewa uraia wa Tunisia na kuchezea katika kikosi cha Tunisia.
Kizazi cha sasa cha Wafaransa kina wachezaji weusi wa aina mbili. Kuna wachezaji waliozaliwa na wazazi wa Kiafrika pale Ufaransa, pia kuna wachezaji ambao walikwenda wakiwa wadogo na wakapewa uraia. Hawa ndio kina Patrick Vieira na Patrice Evra. Ni kitu cha kawaida kwa wenzetu.
Kuna Wanariadha wa Kenya ambao wamewahi kupewa Uraia katika nchi za falme za Kiarabu kwa ajili ya kuwakilisha mataifa hayo. Hiki sio kitu cha ajabu. Hata Morrison akiomba hakiwezi kuwa kitu cha ajabu. Watanzania wanadhani ni kitu cha ajabu kwa sababu wengi kati yetu hatujasafiri vya kutosha na kwenda nchi za watu ambazo utagundua jambo hili ni la kawaida. Hata hivyo, licha ya Morrison kutaka apewe uraia bado kuna mambo ya msingi ambayo inabidi tuyajadili. Wakati fulani watu walitaka staa wa zamani wa Azam, Kipre Tchetche apewe uraia wa Tanzania ili aisaidie timu ya taifa.
Ukweli ni taifa letu halitaweza kuondoka hapa lilipo kusonga mbele kisoka kwa sababu ya kuwapa watu uraia waisaidie timu ya taifa. Kufikia hatua ya Morrison kutamani kuichezea timu ya taifa ni kwa sababu anaiona namba yake katika kikosi cha timu ya taifa.
Wakati fulani niliwahi kusema Morrison anaweza kuchezea timu zote za taifa za ukanda wa Afrika Mashariki. Nadhani hata yeye mwenyewe ameona hivyo. Hata hivyo, kwa upande wetu kuwapa wachezaji uraia sio suluhusho.
Inabidi tuanze kutazama ni wapi tumejikwaa. Zamani wachezaji kama Morrison tulikuwa nao wengi. Siku hizi wametoweka. Kama ni mawinga tu ambao wanaweza kukaa na mpira na kukufuata usoni tulikuwa nao kina Celestine ‘Sikinde’ Mbunga, Edibily Lunyamila, Hussein Mwakuruzo, Justin Mtekere, Omary Hussein ‘Keegan’ na wengineo wengi.
Wamekwenda wapi wachezaji wa namna hii? Imefika mahala sasa Simba wamemtambulisha mshambuliaji wao mpya, Habib Kyombo lakini mashabiki wao wanalalamika. Wanataka watangazwe mastaa kutoka nje. Muda si mrefu jambo hili litahamia katika timu ya taifa.
Tujiulize tulijikwaa wapi? kuna mambo mengi kwa wakati mmoja. Klabu hazitengenezi tena wachezaji wa namna hii. Serikali kupitia michezo wa mashuleni nayo haitengenezi tena wachezaji wa namna hii. lakini wachezaji wenyewe nao hawajitengenezi kufikia hatua kama za wachezaji wa zamani.
Aliwahi kuniambia baba yangu, Sunday Manara ‘Computer’ tofauti kati ya wachezaji wa zamani wa enzi zao na wachezaji wa sasa ni kujituma tu. vipaji ni vile vile tu. Tofauti ni wachezaji wa siku hizi wanacheza kwa asilimia 40 ya uwezo wao, lakini wao walikuwa wanacheza kwa asilimia 90 ya uwezo wao.
Tunawajua wachezaji wetu wenye vipaji vikubwa lakini hawapendi kujihangaisha. Hawa ndio wamewapa akina Morrison viburi vya kuitamani timu ya taifa. Morrison angekutana na mtu anayeitwa Edibily Lunyamila kamwe asingetamani kuichezea timu taifa.
Matokeo yake leo Simba na Yanga zinategemea wachezaji wa kigeni zaidi. ukifuatilia usajili wa msimu huu hata timu nyingi za kawaida zimeanza kuhamia huko. Ni mwendo wa wachezaji wa kigeni tu. Hauwezi kuzilaumu klabu kwa sababu zinataka mafanikio. Simba walipomsajili Yusuph Mhilu walidhani angeweza kufika walau nusu ya Luis Miquissone. Haijatokea. Lakini ukitaka kuona tunaenda gizani unaweza tu kupima kwamba mpira ambao Mrisho Ngassa alicheza katika umri wa Denis Nkane ulikuwa mkubwa zaidi.
Morrison anaweza kuichezea timu ya taifa ya Tanzania lakini sio suluhisho la matatizo yetu. Kuna mahala tumekwama kama taifa na hatuzalishi tena vipaji vya uhakika kama ambayo tulikuwa tunafanya zamani.
Wakati nakisikia tunalazimisha kuwasaka kwa tochi wachezaji wenye asili ya Tanzania ambao wanacheza Ulaya. Hawa nao sio suluhisho la shida zetu. Turudi katika misingi yetu. Tuzalishe wachezaji wanaojitambua na kufanya kazi ngumu.
Tunao akina Morrison kibao lakini ambao kwa bahati mbaya wanacheza asilimia 40 tu ya uwezo wao. Bahati nzuri kwao katika miaka ya karibuni wanapata fedha nyingi zaidi kitu ambacho kinawafanya wasijitume sana.