Jicho la Mwewe...Je Haji Manara Angeweza Kumfokea Tenga?


ALIWAHI kuniambia rafiki yangu fulani hivi akimzungumzia Leodeger Chilla Tenga, rais wa zamani wa TFF. “Anaweza hata kuongoza nchi. Ana hekima, hadhi na busara.” Ni kweli. Nyakati zimepita na sasa wote tunaweza kumkumbuka Tenga alikuwa mtu wa namna gani.

Siwezi kuamini kama Haji Manara angeweza kumsogelea Tenga na kumnyooshea kidole au kumfokea. Hakuwahi kutokea mtu huyo katika mpira licha ya kwamba soka ni mchezo wa kihuni. Kuna watu inabidi uwapishe na kulalamika kimyakimya.

Popote alipojitokeza hadharani Mzee Tenga watu tulitabasamu na kumpa mkono. Kuna na hisia za ‘kumissiana’ baina ya pande zote mbili. Kati ya yeye na watu wake. Au yeye na sisi washikadau. Kusingetokea tukio la kihuni kama lile ambalo limetokea kule Kaskazini mwa Tanzania. Baada ya tukio la Haji Manara na Rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia pale Arusha kuna mambo mengi yamenitafakarisha kuhusu soka letu na watu wake. Haji amefungiwa na anastahili kufungiwa. Haji ni msela tu wa Kariakoo lakini maeneo mengine hatupaswi kuwa na watu wasela.

Labda tuanze kumsema Haji. Inajulikana kuwa amefanya makosa. Makosa haya hakuanza juzi wala jana. Kuna wakati anatoka nje ya mstari. Ni kama alivyotoka nje ya mstari pale Arusha. Lakini tangu akiwa na Simba alishawahi kutoka nje ya mstari. Na sasa yupo ndani ya Yanga huwa anatoka nje ya mstari. Nawashangaa watu wa Simba ambao leo wanamuona Haji kama vile anafanya jambo geni katika soka letu wakati walikuwa naye. Na nawashangaa watu wa Yanga jinsi ambavyo wanamshangilia Haji kama vile anafanya jambo geni wakati majuzi tu walikuwa wanalia naye. Ni namna fulani ya unafiki uliojengeka katika soka letu. Lakini pia ni namna fulani ya Usimba na Uyanga ambao hauwezi kumalizika. Kila kitu tunakiangalia kwa jicho la Usimba na Uyanga. Lakini pia huu ni wakati wa kumjadili Rais wa TFF, Mheshimiwa sana, Wallace Karia. Rais Karia lazima awe makini na mienendo yake. kwanini anafikika kiurahisi? Kwa sababu anaongea kiurahisi. Anaonekana kiurahisi. Anashindwa kuzuia mdomo wake na kuufanya uwe wa Kidiplomasia zaidi. Baadhi ya watu wa TFF huwa wanakuwa na hofu pindi Karia anapoongea na vyombo vya habari.

Kitu gani alichozungumza kuhusu Tundu Lissu? Alivuruga muonekano wote wa taasisi ambayo imekuwa ikihudumia watu bila ya itikadi zao za kisiasa. Lakini hata katika sakata zima dhidi ya Haji, Rais Karia alisikika akimwambia Haji “Wewe nitakufungia mimi”. Hii sio sawa. Anayefungia sio Karia. Haji anapaswa kufungiwa kwa mujibu wa sheria na kamati inayohusika.

Ni vile muundo wenyewe wa hizi kesi huwa haueleweki lakini Karia na Haji wote walipaswa kupelekwa katika kamati ya maadili. Ina maana siku nyingine kama kiongozi wa TFF akikutukana hadharani na kisha mkaishia kutukanana bado anayepelekwa katika kamati ya maadili ni mtu mmoja?

Haji analalamika kwamba Karia ndiye ambaye alimuanza katika sakata zima la Arusha. Huo upande wa Karia kumuanza mtu nani huwa anautazama? Ina maana haki itakuwa inatendekea kwa upande mmoja tu kwa vile viongozi wa TFF hawagusiki? Tukiachilia jambo hilo ebu tujadili kidogo kuhusu adhabu yenyewe. Nadhani adhabu ya Haji inaweza kuwa ndogo zaidi kulinganisha na adhabu ambazo zimeshatolewa hapo awali. Kuna akina Mbwana Makatta na Shaffih Dauda ambao walifungiwa miaka mitano kwa makosa mbalimbali. Mbona inaonekana kitu rahisi sana kumfungia mtu kwa miaka mingi kwa makosa ya kawaida? Kwa mfano Shaffih. Alikosoa tu kwa maandishi kuhusu mfumo wa uendeshwaji wa Ligi. Adhabu yake kwanini iwe miaka mitano? Alitukana mtu? Alimpiga mtu? Hapana. Alitoa maoni yake tu. Hata kama yanakera adhabu yake ni kufungiwa miaka mitano? Naweza kukubali adhabu ya Makatta kama kweli alithibitika kushawishi mchezo wa soka usichezwe. Mara zote kuanzia Fifa mpaka chini adhabu yake inakuwa kubwa. Kuzuia mechi isichezwe kunaharibu taswira kubwa katika mchezo wa soka. Hata hivyo adhabu ya Makatta imepunguzwa mpaka miezi sita. Lakini kifungo kama hiki kingeweza kutolewa tangu awali. Unaposhangaa kuona kifungo kinapunguzwa miaka mitano hadi miezi sita unajua tu kwamba awali wafungaji walimfunga Makatta kwa kumkomoa. Kama walikuwa na uhakika na wanachokifanya basi kifungo cha Makatta kingeweza kupunguzwa kutoka miaka mitano hadi mitatu. Lakini kutoka miaka mitano hadi miezi sita ni wazi kwamba alikuwa anakomolewa. Ni kama ilivyo kwa Shaffih inaonekana alikuwa anakomolewa. Haji naye amekomolewa. Ukitaka kujua hili napenda kuweka utabiri wangu kwamba wote hawa hawatamaliza vifungo vyao. Itatokea namna tu ambayo wataachiwa. Watu hatari katika soka letu ambao wanapaswa kupewa vifungo virefu ni wapanga matokeo ya mechi. Hizi ndio adhabu ambazo zinastahili watu kufungiwa miaka mitano au kifungo cha maisha. Lakini kubishana au kutoleana maneno machafu na Rais hadharani hakupaswi kutolewa kifungo kirefu kama vile mtu amepanga matokeo ya uwanjani. Tupunguze kuishi kisela katika soka. Lazima kuwepo na kuheshimiana baina ya mtu na Taasisi au baina ya Taasisi na Taasisi. Tumeanza kuurudisha mpira wetu katika usela ndio maana akina Haji wameweza kufokeana na Rais wa mpira mbele ya wageni wake. Kwa tunaomkumbuka Rais Tenga aliweka mipaka mingi kati yake na watu wake, lakini pia kati yake na washikadau wengine wa mchezo huu. Wote tulijikuta tunamuheshimu Tenga kwa sababu hatukujua upungufu wake.

Nakubali njia ambayo Katibu Mkuu wa TFF, Wilfried Kidau amechagua kuishi. Kazi zinaendelea lakini ameziba mdomo wake kwa kiasi kikubwa. Katibu ni mtu aliyejitoa katika picha, lakini angeweza kujiingiza katika picha kila siku kwa sababu yeye ni mtendaji. Ameamua kuwa tofauti.

Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad