Jinamizi la Ajali Lazidi Kutafuna Watu



Arusha/Simiyu. Jinamizi la ajali za barabarani limeendelea kugharimu maisha ya watu baada ya watu 16 kupoteza maisha ndani ya siku mbili, ikiwamo ya ndugu wawili na mtoto wa mwaka mmoja iliyotokea mkoani Arusha jana.

Watu hao 16 walifariki dunia katika ajali za barabarani zilizotokea jana na juzi jijini Arusha, Simiyu na Kagera.

Ajali ya Arusha ilitokea Barabara ya Afrika Mashariki inayopita kata Muriet Mashariki ikihusisha gari kugonga ndugu watatu na kukimbia na hadi jana lilikuwa bado halijakamatwa.

Waliofariki ni mtoto Ebenezer Mollel (1), Neema Mollel (27) na Agostino Mollel (24) ambaye alikuwa akiendesha bodaboda.

Kamanda wa Jeshi la Polis Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alisema uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea ili kubaini gari lililohusika ili kufikishwa katika mkono wa sheria. Ndugu hao wamepoteza maisha ikiwa ni siku moja imepita tangu ajali nyingine iliyotokea Barabara Kuu ya Lusahunga kwenda Nyakahura wilayani Biharamulo Mkoa wa Kagera na kuua watu wanane, wakiwamo watano wa familia moja.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia juzi, ikihusisha gari kubwa la mizigo aina ya Mercedes Benz lililokuwa likiendeshwa na Vicent Gakuba (52), raia wa Rwanda kugongama na Toyota Succeed.

Wanafamilia waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ni Jesca Ntahimula (45) na watoto wake wanne Magreth Kimuna (14), Adidas Sekanabo (12), Zabloni Sekanabo na (6) Vedastina Sekanabo (8).

Wengine ni Nyawenda Bisalo (35), Majaliwa Maige (32) na Michael Charles (28).

Ajali nyingine ni iliyotokea juzi usiku mkoani Simiyu na kusababisha vifo vya watu watano na wengine 11 kujeruhiwa eneo la Magereza, nje kidogo ya mji wa Bariadi.

Ajali hiyo ilihusisha magari mawili ya abiria aina ya Toyota Pro box na Toyota Wish zilizogongana uso kwa uso. Kufuatia mfululizo wa ajali hizo za magari madogo maarufu michomoko, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila amepiga marufuku kutoa huduma mkoani humo. Imeandikwa na Mussa Juma, Amina Ngahewa na Samirah Yusuph.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad