Kafulila amshukuru Rais Samia, awaaga wananchi wa Simiyu




 
Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuachwa katika mabadiliko ya wakuu wa mikoa, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu, David Kafulila amemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kumpa nafasi ya kulitumikia taifa.

Alhamisi Julai 28, 2022, Rais Samia alifanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa ambapo amewateua wapya tisa, amewabadilisha vituo baadhi yao na wengine wakibaki katika vituo vyao vya kazi.

Katika mabadiliko hayo, wakuu wa mikoa tisa wameachwa na nafasi zao kuchukuliwa na wengine, miongoni mwa walioachwa ni pamoja na Kafulila.

Wengine ni Ally Hapi (Mara), Robert Gabriel (Mwanza), Steven Kagaigai (Kilimanjaro), Charles Mbuge (Kagera), Wilbert Ibuge (Ruvuma), Marco Gaguti (Mtwara), Joseph Mkirikiti (Rukwa), Binilith Mahenge (Singida).


 
Akizungumza na Mwananchi, Kafulila amemshukuru Rais Samia na kuwaaga wananchi wa Simiyu huku akiwataka wampe ushirikiano mkuu wa mkoa mpya, Dk Yahya Nawanda na kuendeleza walipokuwa wamefikia.

“Kwanza nitoe shukran za kipekee kwa Mhe. Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kumsaidia katika nafasi ya Mkuu wa Mkoa. Ni heshima kubwa kwangu ambayo sikuwahi kuipata hapo kabla.                          

“Pili, ni kuwatakia heri wana Simiyu wote na kuwaomba waendeleze yote tuliyofanikisha pamoja na mengine zaidi ambayo hatukuweza kufanya ambayo watafanya na RC mpya. Binafsi nitaendelea kuitumikia nchi yetu kwa nguvu ile ile kama raia mwema.

“Natoa wito kwa wana Simiyu Kushirikiana RC mpya na zaidi kuendelea kumuunga mkono Rais wetu katika kazi kubwa anayoifanya ya kujenga Mkoa wetu wa Simiyu hasa kwa mapinduzi ya zao la pamba na miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa kila kona ya Mkoa,” amesema Kafulila.

Amewataka wananchi wa Simiyu kuendelea kumuunga mkono Rais Samia katika kufanikisha maono ya kujenga Taifa mpya na kujenga mkoa wa Simiyu hasa katika mapinduzi ya zao la pamba na miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa kila kona ya mkoa.

“Waendelee kumuunga mkono Rais wetu kufanikisha maono makubwa ya kujenga Taifa moja kubwa kiuchumi na hivyo kisiasa ma kujenga jamii kubwa ambayo kila mmoja anayo fursa ya kushiriki ujenzi bila kujali tofauti hizo,” amesema Kafulila.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad