STRAIKA Meddie Kagere amekuwa mmoja wa mastraika wa kwanza wa Simba wanaotajwa kupigwa chini, lakini upepo umebadilika baada ya kuwagawa mabosi wa klabu hiyo katika makundi mawili, upande mmoja ukitaka aondoke na mwingine asalie kikosini.
Habari za ndani kutoka kwa viongozi wa juu wa Simba zinaeleza kuna mabishano juu ya kumuacha Kagere huku wengine wakitaka abaki kutokana na rekodi yake ya mabao aliyoyafunga ndani ya misimu minne.
Ndani ya misimu hiyo, Kagere amefunga jumla ya mabao 65 kwenye Ligi Kuu Bara, tangu alipojiunga msimu wa 2018/19 aliomaliza na mabao 23, kisha kuongeza mengine 22 msimu wa 2019/20 na msimu uliopita wa 2020/21 alifunga 13 na ligi iliyomalizia hivi karibuni alitupia saba.
Jambo hilo baadhi ya viongozi wa Simba wamelikalia kidete kutokukubaliana na mpango wa kuondolewa kwa straika huyo na kuupinga usajili wa Habibu Kyombo aliyemaliza ligi na mabao sita msimu huu akiwa Mbeya Kwanza iliyoshuka daraja.
“Rekodi ya mabao yake 65 inambeba na ngumu kumhukumu wakati timu nzima haikuwa vizuri kwa msimu huu, hivyo mabishano yanayoendelea kumhusu Kagere ni mazito na sijui kama yataisha leo ama kesho,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Ukiachana na Kegere, kuna John Bocco na Chris Mugalu mwanzo walionekana wana nafasi kubwa ya kusalia, lakini kuna watu hawakubaliani nao, wapo wanaotaka waondoke na wanaotaka wabakie, hivyo washambuliaji hao watatu wanapasua vichwa.”
Bocco, Kagere na Mugalu bado wana mkataba wa mwaka mmoja kila mchezaji unaowafanya wazue mjadala wa namna ya kuwaacha na kuwagawa viongozi.
Hadi sasa Simba imesajili washambuliaji watatu wa kigeni wawili ambao ni Augustino Okra, raia wa Ghana na Ceasar Lobi Manzoki kutoka DR Congo pamoja na mzawa Habibu Kyombo huku usajili wao ukielezwa kuwa unaendelea.