Kanisa lafanya tambiko baada ya mwanamume kufa madhabahuni
NA MWANGI MUIRURI
SHUGHULI ya kutakasa African Independent Pentecostal Churches of Africa tawi la Kenol, baada ya mwanamume kufa katika madhabahu ya kanisa hilo Jumatatu, imeanza.
Tambiko hilo litahusisha siku tatu za maombi na kufunga, kumchinja mbuzi mwenye rangi moja, kuliweka kanisa wakfu kwa Kristo kupitia maji na mafuta yaliyotakaswa na kuchoma ubani ili kutakasa eneo hilo.
Askofu Mkuu Fredrick Wang’ombe alizuru kanisa hilo Jumatano na kutangaza siku tatu za maombi na mfungo hadi Jumamosi saa tatu asubuhi wakati ibada ya utakaso itakapoendeshwa kuambatana na mafunzo ya kanisa hilo.
Bw Njoroge Muikamba 28, fundi wa kuchomelea vifaa kwa stima alikuwa akifanyia ukarabati paa la kanisa hilo na anakisiwa kuwa mlevi.
Aliteleza na kuanguka kina cha urefu wa futi 35 kabla ya kugonga kichwa kwanza kwenye madhabahu na kufa papo hapo.
Askofu Wang’ombe alitangaza ibada maalum ya maombi na kufunga.
Aliandamana na Katibu Mkuu wa AIPCA, Kimaru Maina, ambaye pia ni mwenyekiti wa kanisa hilo la Kenol.
Akifafanua matukio yatakayofanyika katika tambiko hilo la utakaso, Bw Maina alisema mzee wa kanisa atamchinja kondoo nje ya kanisa na damu itakayomwagika itawakilisha utakaso wa nuksi ya kifo cha binadamu ndani ya kanisa.
“Baada ya nyama ya kondoo huyo kupikwa, itagawanywa miongoni mwa viongozi wa makuhani na washirika wa kanisa hilo kama sehemu ya kufunga sadaka ya utakaso, na uovu huo kufutiliwa mbali,” alisema Bw Maina.
Kisha, Askofu Wang’ombe ataongoza ibada kuu ya sakramenti takatifu na kutangaza kanisa hilo kuwa huru kutokana na mapepo.
Miongoni mwa Waisraeli, kitendo cha kukata koo ya mnyama na kumtazama akikata roho ni kielelezo cha matokeo ya kutamausha ya dhambi na ubinafsi.
Kifo cha mnyama ni kiashirio cha matokeo ya dhambi yanayojitojeza kwa hofu ya kifo kwa wale wanaotafuta kusamehewa.
“Kifo cha mnyama hutumika kama kielelezo mbadala cha uchungu na mateso yatakayomkumba binadamu,” alifafanua Bw Maina
Madiwani wa zamani wataka marupurupu yao