HUKO Jangwani sasa ni mwendo wa fedha tu. Ndio, wakati ikiendelea kufurahia mikwanja iliyokusanya msimu uliopita pamoja na kutwaa mataji matatu, neema imeendelea kuiangukia klabu ya Yanga baada ya jana kusaini dili tamu la Sh12 bilioni na Kampuni ya SportPesa.
Dili hilo jipya la miaka mitatu, linazidi kuifanya Yanga iogelee kwenye fedha na kama itakomaa tena kwenye michuano itakayoshiriki msimu ujao, itazidi kukusanya mkwanja wa maana kutoka kwa wadhamini waliopo klabuni hapo ikiwamo SportPesa na Kampuni ya Azam Media.
Mapema jana mchana Yanga, chini ya Rais Injinia Hersi Said ilisaini mkataba mpya na SportPesa baada ya ule wa awali wa miaka mitano kumalizika, huku dau likiwa limeongezeka maradufu.
Katika mkataba wa kwanza ambao SportPesa pia iliingia na Simba, klabu ya Yanga ilivuna kiasi cha Sh5.2 bilioni kwa miaka mitano, lakini kitendo cha kuchukua mataji matatu msimu uliopita yaani Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na ASFC, kimeipa mkwanja wa maana kutoka kwa wadhamini.
Mataji mawili tu ya Ligi Kuu na ASFC, Yanga imekomba Sh700 milioni kama bonasi kutoka kwa wadhamini wao wa Ligi Azam Media waliotoa Sh500 milioni, na NBC kutoa Sh100 milioni nas SportPesa kuwakabidhi jana Sh100 milioni.
Ukija wenye ASFC, Yanga imelamba zawadi ya Sh50 milioni za ubingwa, huku kwenye dili la Azam Media la kurusha maudhui, ilikomba Sh2.4 bilioni na uhakika wa kupata bonasi ya Sh4 bilioni kwa kuwa bingwa kwani mkataba huo wa miaka 10 wenye thamani ya Sh 41 bilioni unasema Yanga ikimaliza nafasi ya kwanza au ya pili basi itapata bonasi ya Sh44.4 bilioni kwa miaka 10, ikiwa na maana kila msimu ikimaliza ndani ya nafasi hizo inabeba Sh4.4 bilioni.
DILI LA SPORTPESA
Mkataba mpya wa Sportpesa uliosainiwa jana wa miaka mitatu, Yanga itavuna kiasi cha Sh12.033 bilioni, ikiwa na maana kila mwaka itakomba kitita cha Sh4.011 bilioni.
SportPesa itatoa bonasi kwa Yanga kama itabeba ubingwa wa Ligi Kuu kutoka Sh100 milioni hadi Sh150 milioni, pia kwenye michuano ya ASFC, ikitinga fainali tu itakomba Sh75 milioni na kama itateba kabisa taji itakuwa na uhakika wa kubeba Sh112 milioni.
Hii ina maana kama Yanga itatetea mataji hayo mawili kwa msimu ujao, itakuwa na uhakika wa kuvuna fedha zaidi ukichangana na zile za wadhamini wa ligi NBC na Azam Media ambao wanaidhamini pia Kombe la ASFC na kwa hesabu za haraka itakusanya jumla ya Sh 862 milioni, mbali na ile bonasi yao kutoka Azam kwenye mkataba wa maudhui.
MSIKIE TARIMBA
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa, Tarimba Abbas alisema haikuwa kazi rahisi kwa pande hizo mbili kuingia mkataba huo kutokana na kupanda kwa thamani ya Yanga baada ya kuchukua mataji msimu uliopita.
“Tulipoingia hapa Tanzania mara ya kwanza mwaka 2017 na kuingia udhamini na klabu kubwa za Simba na Yanga mbali na kufanya biashara tulijipambanua katika kuendeleza maendeleo ya soka,” alisema Tarimba aliyewahi kuwa Rais wa Yanga miaka ya mwanzoni mwa 2000 na kuongeza;
“Wote tunafahamu mafanikio ya Yanga msimu uliopita, ilichukua mataji matatu pia ikiwa haijapoteza mchezo, hivyo ugumu ulianzia hapo huwezi tena kuwapa fedha ambazo uliwapa miaka mitano iliyopita, ulihitaji kuwa na ushawishi mkubwa na maboresho ambayo tumeyafanya katika mkataba huu wa miaka mitatu tuna uhakika Yanga inaenda kufanya makubwa misimu inayofuata.”
Naye Injinia Hersi alisema udhamini huo unaenda kuwa na thamani kubwa kwa Yanga ikiwa pia wameridhika na huduma ambayo SportPesa imekuwa ikiwapa na kuamua kuendelea kuwa wadhamini wakuu.