Kina Mdee wafungua kesi kupinga kufukuzwa Chadema




Dar es Salaam. Waliokuwa wanachama na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee na wenzake 18, tayari wamefungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho.

Mdee na wenzake wamefungua shauri hilo siku 13 baada ya kupata kibali cha mahakama hiyo.

Mahakama hiyo imewaruhusu Mdee na wenzake kufungua shauri hilo Julai 8, 2022 baada ya kukubaliana na hoja zao katika maombi waliyokuwa wameyafungua wakiomba ridhaa hiyo.

Mawakili wa kina Mdee, Ipilinga Panya na Aliko Mwamanenge wameieleza Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti kuwa walifungua shauri hilo jana Alhamisi Julai 21, 2022 na kwamba mpaka jioni lilikuwa limeshasajiliwa baada ya nyaraka walizoziwasilisha mahakamani hapo kufanyiwa ukaguzi na mahakama kujiridhisha kuwa zimekamilika na taratibu zimefuatwa kwa mujibu wa sheria.


 
Katika shauri hilo la maombi ya mapitio ya Mahakama, Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawache wa chama hicho (Bawacha) na wenzake wanapinga uamuzi wa kufukuzwa uanachama uliotolewa na Baraza Kuu la Chadema Mei 11, 2022.

Katika uamuzi huo, Baraza hilo lilitupilia mbali rufaa zao walizozikata wakipinga uamuzi wa awali wa kuwavua uanachama uliotolewa na Kamati Kuu ya Chadema Novemba 27, 2020. Badala yake Baraza hilo liliunga mkono uamuzi huo wa Kamati Kuu.

Kamati Kuu iliwavua uanachama baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kukubali na kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila ridhaa ya chama hicho.


Kufuati uamuzi huo walifungua maombi Mahakamani hapo wakiomba ridhaa ya kufungua shauri la kupinga uamuzi huo, pamoja na mambo mengine wakidai kuwa mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama haukufuata taratibu na misingi ya kisheria kwa kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa.

Mahakama ilikubaliana na maombi yao baada ya kuridhika kuwa walikuwa wamekidhi matakwa na vigezo vya kisheria kustahili kupewa ridhaa hiyo.

Baada ya kupata ridhaa hiyo walitakiwa kufungua shauri hilo ndani ya siku 14 kwa mujibu wa sheria, tangu tarehe ya uamuzi wa maombi ya ridhaa, ambazo zinaisha leo Julai 22, 2022.

Baada ya kukamilisha hatua hiyo, ya kufungua shauri hilo, sasa wanasubiri tatatibu nyingine za kimahakama ikiwa ni pamoja kupangiwa jopo la majaji watakaosiliza shauri lao hilo na tarehe ya kutajwa na Kisha tarehe ya usikilizwaji baada ya taratibu zote kukamilika.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad