Kiongozi Chadema ajeruhiwa kwa visu Arusha




Arusha. Katibu wa Chadema Kata ya Kikatiti, wilayani Arumeru mkoani Arusha, Ephata Pallangyo amelazwa hospitali ya mkoa ya Mount Meru akidaiwa kujeruhiwa kwa kuchomwa visu na vijana wanaodaiwa kuwa CCM.
Tukio hilo limetokea jana Julai 20, 2022 usiku, baada ya vijana wa wanadaiwa ni Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuondoa bendera za Chadema barabara kuu ya Arusha –Moshi na kuanza kupambana na vijana wa Chadema.
Akizungumza katika hospitali ya Mount Meru, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure amesema vijana hao walikuwa wakiondoa bendera kwenye matawi ya chama hicho yaliyo barabarani na licha ya kukataliwa waligoma na kuanza kutumia nguvu.
"Wakati vurugu zinatokea Polisi walikuwepo katika doria barabarani wakisubiri msafara wa Rais Samia Suluhu kupita na tunaimani watalifanyia kazi suala hili," amesema.
Kamanda wa Polisi mkoa Arusha, Justin Masejo jana pamoja maofisa kadhaa wa Polisi walimtembelea mgonjwa huyo hospitali ya Mount Meru, lakini hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
Alipoulizwa kuhusu ushiriki wa vijana wa CCM katika tukio hilo, Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Gerald Munisi amesema hana taarifa za tukio hilo.
"Mimi jana nilikuwa katika msafara wa Rais, sina taarifa za hilo tukio kutokea labda nifuatilie," amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad