NIMELAZIMIKA kuandika hili ili kuweka sawa mambo yanayoendelea nchini baada ya mkuu wa kitengo cha mawasiliano, Haji Manara kukufungiwa miaka miwili na faini ya Sh. milioni 20.
Wengi wanaliangalia suala hili kishabiki; wapo wanaofurahia, wanaosikitika huku wale wenye tofauti na Manara wakichekelea kwamba amekiona cha mtema kuni.
Baadhi wanadai kwamba kama kanuni zinasema faini iwe kuanzia Sh. milioni 3, kamati iko sahihi kutaja kiasi chochote. Sijui kamati ingesema faini ya Sh. bilioni 20 wangeafiki? Ni lazima kuangalia kila jambo katika picha kubwa na si kuangalia leo tu au yule linalomuathiri pekee.
Hii si mara ya kwanza kwangu kuzungumzia adhabu za namna hii. Niliandika wakati Shaffih Dauda alipofungiwa miaka mkitano; niliandika wakati wa Fred Mwakalebela; wakati Katabaro alipofungiwa maisha kujihusisha na soka ‘eti’ kwa sababu alihoji uhalali wa wajumbe wa mkutano wa uchaguzi Ubungo na nilihoji wakati wa Mbwana Makata aliyetaka kanuni za ligi kuhusu gari la wagonjwa kuwepo uwanjani ziheshimiwe.
Ni adhabu chache hadi sasa zinaendelea. Ile ya Shaffih kwa sababu hajalamba miguu watu na ile ya Katabaro ambaye bado anapambana na uonevu. Ile ya Mwakalebela iliisha baada ya vikao na wizara; ya Makata imepunguzwa hata kabla ya miezi miwili, ya Bumbuli iliisha kiajabu, ya kwanza ya Manara iliisha kwa kulipa faini. Hapo kuna nia ya dhati ya adhabu hizo? Labda kinachotakiwa kwao ni kulamba miguu watu baada ya kutangaziwa adhabu kubwa.
Kwa hiyo napozungumzia suala la Manara, sizungumzii kwa sababu ni Haji au kwa sababu ana mrengo fulani, bali ni kwa kuliangalia suala lake katika picha kubwa zaidi ya tukio analodaiwa kulifanya.
Awali niliona kama Kamati ya Maadili imekaririshwa adhabu, lakini baadaye nimegundua kanuni za maadili zimewekwa kwa njia ambazo kamati inalazimika kufungia na kulipisha faini. Kwenye maeneo ambayo kanuni tulizoziiga Fifa zinasema adhabu za ujumla ni kuonya, kufungia, kuzuia kuingia uwanjani, kuzuia kukaa benchi na nyingine hadi kufungia, sisi tumechakachua. Tumeongeza kasentensi kanakoelekeza mtumiaji wa kanuni aende kifungu cha 73 ambako kuna hizo adhabu.
Kumbe kanuni tulizoiga za Fifa zinasema kamati “inaweza” kutumia adhabu iliyoidhinishwa katika kifungu 7(j), ambacho kinaelekeza kufungia. Lakini kifungu hicho kinaendelea kusema kuwa adhabu hiyo itaambatana na muda wa uangalizi (probation) wa kuanzia mwaka mmoja hadi mitano. Pia kinasema “iwapo katika muda huo, mshtakiwa atarudia kosa lake au kufanya jingine lolote linalokiuka kanuni hizi za maadili”, ataondolewa faida ya kuwa chini ya uangalizi na hapohapo adhabu yake ya kufungiwa itaanza kutekelezwa. Haya ni mambo ambayo hayasemwi na badala yake watu wamekariri kwamba “ili mradi kanuni zinasema, hakuna tatizo”. Huo ni ukasuku. Ni lazima tujifunze kuhoji.
Kitendo cha kufungia watu wa mpira kila mara hakilengi kurekebisha watu bali kuwatishia ili wasalimu amri, wanyenyekee, au wote wawe chawa! Hatuwezi kuendelea kwa jinsi hiyo. Hata pale kanuni za Fifa zinapoelekeza kamati kuzingatia mambo kadhaa kabla ya kutoa hukumu, sisi tumeengua hayo maneno ili kuwe na sababu kwamba hakuna kitu kama hicho.
Kwa hiyo, hukumu ya Manara imesaidia kujua mengi zaidi kuhusu uendeshwaji wa mashauri yanayowasilishwa mbele ya Kamati ya Maadili na Maamuzi.
Fifa ndiyo yenye mchezo na hivyo imetengeneza kanuni hizo kulingana na utamaduni wa mpira. Kitendo cha sisi kuchakachua kinatufanya tutofautiane na wengine. Kwanza tuheshimu maadili kwa kuondoa uchakachuaji wa kanuni ndipo tuadhibu wanaozivunja.