No title



KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi ametimka nchini juzi mchana na ndege iliyomleta kiungo wake mpya Gael Bigirimana, lakini akafichua kiungo mshambuliaji Aziz KI ni mwananchi rasmi na ataonekana kuanzia leo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi aliyechukua tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2021-2022, alisema anaondoka akijua Aziz KI ni mchezaji mali ya Yanga baada ya kumalizana na mabosi wa klabu hiyo na kuanzia leo ataonekana rasmi.

Nabi alisema usajili huo ni moja ya kazi bora ya Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said akisema raia huyo wa Burkina Faso ni mmoja kati ya watu bora ambao wataiongezea thamani kubwa Yanga msimu ujao.

“Naondoka, lakini nina uhakika Aziz KI ni mchezaji wa Yanga, kwa sasa akili yangu inawaza jinsi gani nimtumie kule mbele, hicho ndio kitu ambacho kipo kwenye akili yangu, mtamuona hapa kuanzia kesho, mtamuona subirini,”alisema Nabi na kuongeza;


“Hii ni zawadi kubwa kwa mashabiki wa hii klabu, ni kazi bora ambayo Hersi (Said) aliifanya nimefurahi uamuzi wa wanachama kumchagua jana (juzi), ni kijana anayepigana kwa ajili ya hii klabu sio rahisi kumpata mchezaji kama huyu kuja kucheza Tanzania.”

BIGIRIMANA SASA

Aidha, Nabi mbali na usajili wa Aziz KI ambaye ni staa wa zamani wa ASEC Mimosas, alisema pia usajili mwingine bora utakaoifanya Yanga iwe bora ni ujio wa kiungo Mrundi Gael Bigirimana.

Nabi aliyeiongoza Yanga kucheza mechi zote za mashindano kuanzia Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la ASFC bila kupoteza alisema, Bigirimana anakuja kuongeza nguvu kubwa katika eneo la kiungo kutokana na ubora wake.


Kocha huyo alisema Bigirimana anakwenda kuongeza ubora mkubwa wa kikosi chake sambamba na uwepo wa viungo wengine Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Khalid Aucho, Zawadi Mauya na Feisal Salum ‘Fei Toto’.

“Wakati tumepata taarifa tunaweza kumpata Bigirimana nilimuomba Mungu tufanikiwe hii muvu, hatukuwa na kiungo wa aina yake anayejua kutengeneza muunganiko wa eneo la kiungo la kati,” alisema Nabi na kuongeza;

“Naona watu wanazungumzia juu ya kwanini hajafunga huko Ulaya, sioni kama ni akili sawasawa ya kujadili kuhusu mtu bora kama huyu,najua jinsi ya kumtumia Bigirimana hapa ili Yanga iwe timu ya hatari zaidi.

“Tuna Sure boy, Aucho, Feisal na Mauya lakini ubora mkubwa wa hawa watu wanne tunaongeza na nguvu ya Bigirimana, ni mchezaji mzoefu anayejua kutengeneza ugumu mkubwa wa eneo letu la kiungo, roho yangu sasa imetulia kwa huu usajili.”


Bigirimana alitambulishwa juzi kwenye uchaguzi wa Yanga baada ya awali Mwanaspoti kuwahabarisha angetua nchini na kufanikiwa kumpata wakati alipowasili Ijumaa mchana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad