KABLA giza halijaingia leo, Yanga itakuwa imemshusha jijini Dar es Salaam, staa wake mpya, Stephane Aziz KI, Mwanaspoti limejiridhisha.
Taarifa kutoka nchini Burkina Faso ni kwamba KI ameondoka kwao jana na kwamba leo atakuwa nchini tayari kwa utambulisho rasmi kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo sambamba na kufuta tetesi zilizokuwa zimeenea kwamba anatua Simba au Azam.
Mwanaspoti ilikuthibitishia awali kwamba staa huyo atatua Yanga na sasa ni wazi kwamba ujio wa KI utamrahisishia mgombea pekee wa nafasi ya Urais wa Yanga, Hersi Said katika Uchaguzi Mkuu wa Klabu hiyo kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere kesho.
Hersi akiwa makamu mwenyekiti wa kamati ya mashindano alizipiga bao klabu za Simba na Azam na nyingine nyingi za Afrika Kaskazini ambazo zilikuwa zinawania saini ya mshambuliaji huyo wa zamani wa mabingwa wa Ivory Coast, Asec Mimosas.
Azizi KI anatua leo akifuatana na mama yake mzazi ambaye ni meneja wake tayari kwa kusaini dili la miaka miwili. Kinachowakera Simba kwa KI ni kwamba msimu uliopita aliwatikisa mara mbili katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Hersi na timu yake watafunga kampeni kwa utambulisho wa Azizi KI sambamba na kiungo Gael Bigirimana ambaye naye anatarajia kutua leo.
Kutua kwa Aziz KI na Bigirimana sasa kutaifanya Yanga kubakisha staa mmoja pekee kuja kutambulishwa ambaye ni beki wa kushoto Mkongomani Lucy Lomalisa.
BIGIRIMANA HUYU HAPA
Mido raia wa Burundi, Gael Bigirimana anayekipiga katika klabu ya Glentoran ya Ireland, atatua nchini muda wowote licha ya kwamba mashabiki wengi mitandaoni wamekuwa hawaamini kuhusu usajili huo. Staa huyo ameridhia kuja nchini kwani hafurahii maisha ya Ireland lakini anataka familia yake ikae kwa muda karibu na Burundi ambako ndiko chimbuko la wazazi wake.
Usajili wa Bigirimana unaifanya Yanga kuweka rekodi ya kuwa klabu pekee iliyowahi kumshusha mtu ambaye amewahi kucheza ligi ya England akiwa na Newcastle United na Coventry City.
Yanga ilikuwa inasaka kiungo mkabaji wa chini lakini mwenye ubora wa kujua kupandisha mashambulizi ya haraka mbele na baada ya msako mrefu wakatua kwa Bigirimana ambaye anajua kazi ya kupambana kwenye kiungo.
BIGIRIMANA NI NANI?
Bigirimana ni mzaliwa wa Burundi akihamia Uingereza na familia yake kama mkimbizi mwaka 2004 na kuchagua kuiwakilisha England (U-20) lakini mwaka 2013 akabadili mawazo na kurejea timu yake ya taifa alilozaliwa ya Burundi 2015 na kucheza Afcon 2019 iliyofanyika Misri.
Nyota huyo aliyezaliwa Oktoba 22 mwaka 1993, aliichezea Coventry City mwaka 2011 kisha 2012-15 Newcastle United ya England na baadaye Rangers ya Scotland kabla ya kurejea tena kwa mkopo Coventry City 2015.
Ana kumbukumbu ya kufunga kwenye mchezo wa Fainali akitumikia Coventry City 2017 na baada ya hapo alijiunga na timu ya Motherwell ya Scottland kisha kuondoka Januari 2019 na kutimkia Hibernian ambapo alidumu muda mchache.