Maajabu ya Somalia straika achukua nafasi ya kipa, ikichezea kwa Stars




Taifa Stars imeanza vyema safari ya kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), baada ya kuichapa Somalia 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa bao lililofungwa na Abdul Suleiman 'Sopu' dakika ya 47.
Dar es Salaam. Taifa Stars imeanza vyema safari ya kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), baada ya kuichapa Somalia 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa bao lililofungwa na Abdul Suleiman 'Sopu' dakika ya 47.

Stars itarudiana na Somalia Julai 30 kwenye uwanja huo huo, matokeo ya mchezo huo ndio yatatoa mwanga wa kusonga mbele zaidi.

Mechi haikuanza kwa kasi kwa timu zote mbili, Lakini Stars ilifika mara nyingi golini kwa Somalia hata hivyo mipango yao ya kufunga haikuwa mizuri.

Viungo wa Stars ambao ni Sure Boy, Mzamiru Yassin na Fei Toto aliyekuwa anapanda kusaidia  kushambulia, walijitahidi kutengeneza mipira ya kuwalisha mastraika George Mpole na Abdul Suleiman 'Sopu'.


 
Spidi ya mchezo ilianza kuonekana dakika ya 17 na kuendelea ambapo Somalia ilikuwa inashambulia kwa kushtukiza.

Dakika ya 31 mshambuliaji wa Somalia, Farhan Mohamed alitengeneza shambulizi la hatari lililowahiwa na beki wa pembeni Kibwana Shomari baada ya kukabwa akatoa pasi iliyoangukia miguuni mwa Bakari Mwamnyeto.

Dakika ya 37 naye mshambuliji wa Stars, Kibu Denis alipata nafasi nje kidogo ya eneo la 18 golini mwa Somalia lakini alipiga shuti lililopaa juu, huku wakati huohuo dakika ya 39, kiungo 'Sure Boy' alimtengenezea shambulizi zuri Fei Toto ambaye alikosea vipimo na mpira ukatoka nje.


Dakika ya 47 ya kipindi cha pili, Stars ilipata bao la utangulizi kupitia kwa kiungo mshambuliaji, Abdul Suleiman 'Sopu' kwa kichwa kilichomshinda kipa wa Somalia, Said Aweys Ali baada ya krosi safi iliyopigwa na beki, Kibwana Shomari.

Dakika ya 83 Stars ilipata ugeni golini kwa Manula ambaye wakati anakwenda kuokoa shuti la Farhan Mohamed alijigonga kwenye goli, kisha akaanguka chini baada ya kuangaliwa na madaktari alibebwa kwenye machela na nafasi yake ilichukuliwa na Aboutwalib Mshery.

Wakati mchezo huo ukiwa dakika za nyongeza Kipa wa Somalia, Said Aweys Ali alishindwa kuendelea baada ya majeraha na nafasi yake kuchukuliwa na  mshambuliaji, Ahmed Hussein Hassan aliyetokea benchi baada ya timu hiyo kumaliza mabadiliko.

Licha ya mshambuliaji huyo kukaa langoni mwake kwa dakika chache ila aliendelea kuonyesha umahiri na kuokoa baadhi ya mashuti likiwemo la Reliants Lusajo.

Dakika za mwishoni Somalia ilijaribu kupambana ili kusawazisha bao, lakini ilishindika, hivyo Stars ikaibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kikosi cha Stars, Aishi Manula, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Kibwana Shomari, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Mzamiru Yassin, Salum Abubakar 'Sure Boy', Abdul Suleiman 'Sopu', Feisal Salum 'Fei Toto', George Mpole na Kibu Denis.

Kikosi cha Somalia ni Said Aweys Ali, Ayman Mohamed Hussein, Isse Abdulkadir Ibrahim, Ahmed Abdullahi Abdi, Anwar Sidali Shakunda, Abdikarim Abdalla Mohamud, Abdulkadir Adan Enow, Farhan Mohamed Ahmed, Yasin Mohamed Osman, Abdiwali Abdirahman Mohamed na Aweys Adan Iman.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad