Waziri wa Nishati Januari Makamba, akizungumza na wafanyakazi wa Tanesco, Bariadi mkoani Simiyu
WAZIRI wa Nishati, Januari Makamba amewataka watumishi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kufanya kazi kwa uhuru na kujiamini, kwani hakuna mfanyakazi yeyote ambaye atafukuzwa kazi kwa kuongea ukweli au uhalisia wa jambo husika.
Amesema kuwa mwelekeo wa serikali kwa sasa ni kuhakikisha Tanesco inaendeshwa kwa ukweli na ufanisi mkubwa, kwa wafanyakazi wake kufanya kazi kwa amani na kujiamini
Makamba ametoa kauli hiyo leo mjini Bariadi mkoani Simiyu wakati akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo katika Ofisi ya Tanesco mkoa, wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani humo.
Waziri wa Nishati Januari Makamba, akizungumza na wafanyakazi wa Tanesco, Bariadi mkoani Simiyu
Amesema kuwa katika mwelekeo huo mpya, hakuna mfanyakazi ambaye ndani ya Tanesco atafukuzwa au kuadhibiwa kwa kusema mambo yalivyo, bali hatua hizo zitachukuliwa kwa mtu mwenye lugha chafu kwa wateja au kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Amesema kuwa anatambua baadhi ya watu watapata shida mwanzoni, akini amewaeleza kila mfanyakazi wa shirika hilo anatakiwa kutambua kuwa huo ndiyo utamaduni mpya.
“ Hakuna mfanyakazi yeyote wa Tanesco atafukuzwa, kusimamishwa kazi au kuadhibiwa kwa kusema mambo yalivyo, usiseme kitu ambacho siyo cha kweli hata siku moja kwa ajili ya kunifurahisha mimi au mwingine, hatutafika, tunataka kuendesha shirika letu katika ukweli,” amesema Makamba.
“Mimi mwenyewe moja ya shida kubwa ninayopata ni kusema mambo yalivyo, ukweli unakufanya ulale usingizi, kwa sababu hakuna kitu kinachohitaji juhudi kubwa kama kuficha ukweli, lazima tuwe wakweli ili mambo yaweze kwenda,” ameeleza Makamba.
Amesema kuwa hakuna haja ya mfanyakazi yeyote kutoa sifa ambazo hazipo, kuficha mambo kuweka sukari kwani huo siyo mwelekeo wa shirika na serikali kwa sasa.