Mtwara. “Bye dady, bye mamy.” Hayo ndio maneno ya mwisho waliyoyatoa watoto wawili wa familia moja waliofariki dunia katika ajali ya basi iliyoua watu 11 wakiwamo wanafunzi tisa, wakiwaaga wazazi wao kabla ya kuondoka nyumbani kwenda shuleni.
Akisimulia kwa uchungu, Stella Yohanna ambaye ni mama wa watoto hao wawili amesema kuwa hiyo ndio ilikuwa tabia yao na asubuhi baada ya kuwaanda walikwenda kumuaga baba yao kabla ya mama huyo kuwapeleka kwenye gari la Shule ya Msingi ya King David.
Stella ambaye ni mkazi wa Mtwara mjini amepoteza watoto wake wawili katika ajali hiyo ambayo imetokea asubuhi leo Jumanne Julai 26, 2022 eneo la Mjimwema, Kata ya Mikindani, Mtwara Mjini wakati watoto wakipelekwa shuleni.
Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa Stella Yohana eneo la Peninsula Mtwara Mjini ambaye amepoteza watoto wake wote wawili Johari (7) na Emmanuel (5) katika ajali ya gari la Shule ya Msingi Msingi ya King David. Picha na Florence Sanawa
Akishindwa kujizuia dhidi ya maumivu aliyonayo, alijikuta akilia na kukumbuka namna alivyoagana na watoto wake pekee kwa mara ya mwisho asubuhi baada ya kuwaandaa.
“Huwa wakiwa wanaondoka huwa wanasema bye dady bye mamy (kwa heri baba, kwa heri mama) hivyo ndivyo wamezoea. Siwezi kuelezea, uchungu wa mwana aujuae mzazi,” amesema
Stella amesema mtoto wa kwanza ana umri wa miaka saba ambaye yuko darasa la kwanza na wa pili (wakiume) ana miaka mitano yupo pre-unity.
Watoto hao huchukuliwa na gari saa 12 hadi saa 12:15 asubuhi jambo ambalo humfanya kuwaamsha na kuwaandaa mapema.
Amesema hadi ajali hiyo inatokea hakuwa na malalamiko juu ya ubovu wa gari wanalotumia watoto huku akieleza kwa siku za nyuma suala hilo liliwahi kutokea.
Akizungumzia chanzo cha ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo alisema ni gari kufeli kwa breki kisha kutumbukia shimoni.
Katembo amesema gari hiyo aina ya Hiace ilifeli breki na kumshinda dereva kisha kuingia kwenye mteremko na kusababisha wanafunzi nane na watu wazima wawili akiwemo dereva kufariki dunia na majeruhi zaidi ya 18.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk Hamad Nyembea amesema amepokea majeruhi 18 kati yao 12 ni wa kike na sita wa kiume.
Amesema majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu huku waliofariki wa kike ni watano, kiume ni watatu na watu wazima wawili.
Mwanachi