Mfumo mikopo elimu ya juu kufumuliwa



 
SERIKALI imeunda timu maalumu ya kupitia mfumo wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu ili kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye sifa anapata huduma hiyo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mwelekeo wa wizara, vipaumbele na maeneo ya kimkakati katika utekelezaji kwa mwaka wa fedha wa 2022/23. PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari.

Alisema lengo la kufanya mapitio hayo ni kuhakikisha mikopo hiyo inatolewa kwa wanafunzi wote wenye sifa na kuondoa urasimu.

“Tumeona kuna kazi nzuri ambayo inafanywa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) lakini tunataka kuendelea kuboresha zaidi utoaji wa mikopo hiyo. Sasa kuna timu ya wataalamu ambayo imeundwa kupitia mfumo mzima wa utoaji wa mikopo hiyo,” alisema Prof. Mkenda.

“Lengo ni kutaka kila mwanafunzi mwenye sifa ya kupata mkopo anayechaguliwa kujiunga na elimu ya juu apate. Hii ni haki ya kila mtu, hivyo tunataka angalau kufahamu kwa kipindi cha miaka mitano namna ambavyo mikopo imekuwa ikitolewa, je vile vigezo ambavyo vinafahamika na wananchi vinafuatwa?


 
“Kwa hiyo tunakaribisha watu watoe taarifa, kwa mfano kama una wasiwasi wowote kuhusiana na utoaji wa mikopo hiyo. Ni vyema uje kutoa taarifa au kama kuna mwanafunzi ulisoma naye na una taarifa zake unakaribishwa. Tunachotaka ni kuhakikisha mikopo inatolewa kwa haki.

“Tunataka kufahamu pia kama kuna ‘room’ (nafasi) ya watu kupiga simu na kusema mwanangu yuko hapo mpe mkopo. Kama kuna nguvu ya watu wenye ushawishi wa kutaka watoto wao wapate mikopo wakati wao wana uwezo wa kulipa pia tujue,” alisema.

Prof. Mkenda pia alisema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ufadhili wa masomo wa Sh. bilioni tatu kwa mwaka huu kwa wanafunzi ambao wamefanya vizuri katika masomo ya sayansi, uhandisi na elimu tiba kwenye vyuo vikuu.


Akizungumzia kuhusu maboresho yanayofanywa katika sekta ya elimu katika eneo la sera, mitaala na sheria, Prof.Mkenda alisema mchakato wa kukamilisha maboresho hayo unahitaji muda wa kutosha ili kuhakikisha kwamba maboresho hayo hayatakuwa ya kukurupuka.

“Mwaka huu bado tunaendelea kupokea maoni ya namna ya kuboresha sera, mitaala na sheria zetu na baada ya hapo, mchakato wa uamuzi utakuwa unatolewa kwa awamu, kikubwa zaidi tunachokwepa hapa ni kukurupuka. Hatutaki kufanya maboresho ambayo tukikaa kidogo yahitaji maboresho mengine tena,” alisema Prof. Mkenda.

Kazi hii ya kuboresha sekta ya elimu ni mpango ambao umeanzishwa na serikali si wa Waziri. Kwa  hiyo ni jambo ambalo ni lazima litakamilishwa,” alisisitiza.

Alisema wizara hiyo bado inakaribisha wadau na makundi mbalimbali kutoa maoni yao katika kufanikisha maboresho hayo kwenye sekta ya elimu nchini.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad