Miili ya watoto 5 wa familia moja yazikwa, chakula walichokula chatajwa



Monduli. Chakula cha mwisho walichokula watoto watano wa familia moja na kusababisha vifo vyao katika kijiji cha Mswakini chini, wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha ni ugali na maziwa ulioandaliwa nyumbani na wazazi wao.

 Watoto hao wa familia moja ya Nyangusi Mollel (45) na Nandoye Nyangusi (32) walifariki dunia kwa nyakati tofauti kuanzia Julai 5 hadi Jumanne Julai 19, 2022 katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Miili ya watoto hao Lemali (8), Sophia (5), Lenendoye (8), Veronica  (11) na Lopoi Nyangusi (6) ambaye alikuwa wa kwanza kufariki dunia imezikwa leo Jumatano Julai 20, 2022 kijijini kwao.

Wazazi wa watoto hao waliokuwa wanashikiliwa jana Jumanne na Jeshi la Polisi Monduli kwa uchunguzi wa tukio hilo linaloelezwa linatokana na kulishwa sumu waliachiwa na kushiriki mazishi ya watoto wao.


 
Wakizungumza na Mwananchi ndugu wa familia hiyo, wamesema chakula hicho, walikula Julai 1, 2022 na baadaye walianza kuumwa na mmoja kukimbizwa katika hospitali binafsi wilayani Karatu na baadaye kufariki.

Watoto wengine wanne pia walianza kuumwa tumbo la kuanza kuvimba kisha walianza kupatiwa matibabu nyumbani na baadaye hali kuwa mbaya, na kupelekwa Hospitali ya Jeshi Monduli (TMA).

Baba mdogo wa watoto hao, Kirong'a Mollel amesema, walipata nafuu lakini wakati wakirejea nyumbani hali zilibadilika ndipo wakapelekwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na baadaye wakafariki.


Mollel amesema chakula kilichowasumbua watoto kilikuwa ni ugali na maziwa ambacho ni kawaida yao kila siku wakitoka  shuleni na machungaji.

"Hatuna chakula kingine pale nyumbani ni ugali na maziwa tu, ndicho walikula na baadaye walianza kuumwa, ndio sababu sisi tunataka uchunguzi zaidi kujua hiyo sumu ilitoka wapi," amesema Mollel

Mwanafamilia mwingine, Leseno Mollel amesema watoto hao, huishi na baba na mama yao pekee ambapo ni familia na mke mmoja na hakuna mgogoro ambao ulikuwepo katika familia hiyo.

Mollel amesema, baba wa watoto hao, Nyangusi Mollel na mke wake, Nandoye Nyangusi walikuwa na watoto saba na mmoja bado ananyonya ambaye amesalimika.


 
"Tumejaribu kuuliza kama kulikuwa na ugomvi nyumbani au kwa majirani, tumeshindwa kujua ukweli nini chanzo cha watoto kuumwa matumbo na kuvimba," amesema

Mwenyekiti wa kijiji cha Mswakili, Nanga Karani amesema tangu walipopata taarifa za ugonjwa wa watoto hao, kabla hawajafariki walihoji wazazi kama kuna dawa wamewapa, walikana.

"Tuliuliza majirani na watu wengine kama kuna kitu kibaya waliona watoto wamekula hatukujua nini kilitokea," amesema

Amesema mtoto aliyesamilika katika familia hiyo ana miaka 12 ambaye hakuwepo nyumbani alikwenda kwa bibi yake na mwingine aliyebaki ana miezi saba bado ananyonya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad