Leo ni siku ya Mitandao ya Kijamii Duniani ambayo huadhimishwa Juni 30 kila mwaka tangu mwaka 2010. Mitandao ya kijamii hutumika na kundi kubwa la watu katika jamii kama sehemu ya mawasiliano, biashara na elimu.
Mitandao maarufu zaidi Tanzania ni Facebook, Whatsapp, Instagram, Youtube, TikTok, Snapchat na Twitter.
Mtandao wa kwanza wa kijamii uliitwa "Six Degrees'' ulianzishwa Mei 1997 na Andrew Weinreich. Mitandao mingine ikafuata kama Friendster (2002), LinkedIn (2003), kisha mwaka 2004 ikaja Orkut, MySpace na Facebook.
Mitandao ya kijamii hutumika katika biashara na ni nyenzo muhimu katika uuzaji wa bidhaa, baadhi ya wateja kabla ya kununua bidhaa hufuatilia sifa na ubora wa bidhaa katika mitandao na kuangalia bidhaa hiyo inatambulika kwa kiasi gani, na maoni ya watu kuhusiana na bidhaa husika.
Kuna mitandao maarufu kama YouTube, LinkedIn na TED hii ni mizuri kwa lengo la kuongeza ujuzi kama unataka kujifunza jambo fulani na inapatikana bure nchini. Kuna maudhui mbalimbali kama ya teknolojia, ufundi, mitindo, upishi, nk.
Kwa wafanyabishara mitandao ya kijamii inawapa nafasi ya kuwasiliana na wateja kwa wakati, kuuza na kutangaza bidhaa na huduma zinazopatikana.
Kujitangaza au kutafuta wateja kupitia mitandao ya kijamii ni njia rahisi na isiyo gharama na inaweza kuwafikia watu wengi zaidi
Mitandao kama Instagram, Facebook na Twitter ina watumiaji wengi nchini na wengine hutumia mitandao hii kwa ajili ya kutafuta bidhaa.
Unaweza kuwa na biashara yako au kampuni yako inayotoa huduma ama bidhaa imara na uhakika kabisa lakini usipotumia bidii kujitangaza ama kujiweka kwenye mitandao, unaweza kuzidiwa na watu ambao huduma zao hazina ubora zaidi yako.
Mitandao ya kijamii ni watu, hivyo kampuni au mfanyabiashara anatakiwa afahamu namna ya kuishi na watu na kuvutia kundi la watu ambao anawahitaji.
Youtube ni mtandao ambao kujiunga ni bure kabisa, lakini pia ni sehemu ya kutengenezea pesa kama utakua unafanya kitu chenye mvuto kwa jamii pamoja na watu unaotaka kuwagusa kutokana na aina ya channel ambayo umefikiria kutengeneza. Muhimu ni kuzingatia vigezo, masharti na sera za mtandao huo