Mkurugenzi wa Jiji la DAR Mikononi Mwa Takukuru

 


WAZIRI MKUU wa Tanzania Kassim Majaliwa, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam Jumanne Shauri, pamoja na watumishi wengine tisa wa jiji hilo.


Waziri mkuu amewasimamisha watumiahi hao ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali, ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 10 zilizokusanywa na hazikuwasilishwa benki kama sheria inavyoelekeza.


Agizo hilo linatokana na matokeo ya ukaguzi maalum kuhusu Mapato ya Ndani katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2020/2021 uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


Watumishi hao pia wamekabidhiwa kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Dar Es Salaam kwa mahojiano juu ya tuhuma zinazowakabili.


Majaliwa ametoa taarifa hiyo leo (Jumatatu, Julai 11, 2022) wakati akizungumza na  viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, Wabunge, Madiwani pamoja na watumishi wa wilaya ya Ilala katika ukumbi wa Karimjee akiwa katika ziara yake ya kikazi Dar Es Salaam.


“Ripoti ya CAG imebaini kuwa wataalamu wa Halmashauri waliohusika na upotevu wa mapato, walikuwa wakiingilia moja kwa moja kati ya mfumo wa LGRCIS na benki, na kuandika kwenye mfumo malipo ambayo hayakufika benki kwa lengo la kuficha ukweli wa kasoro na matumizi ya fedha kinyume cha sheria za fedha za umma. Pia wahasibu waliingiza kwenye mfumo kiasi ambacho hakikupelekwa benki, kwa lengo la kupotosha taarifa halisi za makusanyo.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad