Mnyukano wa Mongella, Gambo mbichi




Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amemjibu ‘kiaina’ Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella aliyedai kuna baadhi ya madiwani wanakwamisha ujenzi wa kituo kipya cha mabasi eneo la Bondeni City na kueleza wasiondolewe kwenye ajenda yao kupambana na wizi jijini Arusha.

Siku chache zilizopita Mongella, katika kikao cha kujadili taarifa ya CAG, aliwataka madiwani wa jiji la Arusha kuacha majungu, fitina na kukwamisha maendeleo ya jiji ukiwepo mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi.

Juzi akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Engutoto, Gambo alisema hakuna anayekwamisha ujenzi wa kituo hicho kama inavyoelezwa bali kinachofanyika ni kuzima hoja ya wizi wa mamilioni ya fedha uliotokea katika jiji la Arusha.

Gambo alisema mjadala wa kituo kipya cha mabasi katika jiji la Arusha, ulifungwa na kitajengwa katika eneo la Bondeni City kama ambavyo Serikali ilitoa maamuzi.


 
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha na mchakato wa ujenzi unaendelea eneo la Bondeni City na hakuna mgogoro na hati ya ujenzi wa eneo hilo ipo hao ambao wanaleta ajenda nyingine wanataka kuchepusha hoja ya wizi wa fedha katika jiji kwani tayari MKurugenzi wa jiji Dk John Pima na wengine wapo magereza.

Gambo alisema wizi uliofanyika katika halmashauri ya jiji la Arusha, unafahamika na waliofikishwa kwenye vyombo vya sheria ni wachache na waliobakia wamepata kiwewe na wanatoa maneno yasiyo na kichwa wala miguu.

Alisema maneno yanayotolewa hayawezi kuwarudisha nyuma kukemea wizi wa fedha za umma.


Gambo alisema fedha ambazo zimeibwa ni nyingi na hivi sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali(CAG) yupo kazini na anaamini akikamilisha kazi yake ndipo itaonekana kwanini leo jiji linakusanya zaidi ya bilioni 23.

Alisema badala ya fedha hizo, kupelekwa kukamilisha ujenzi wa madarasa,mabweni na kukarabati madawati au kupelekwa kwa wakala wa barabara Vijijini (Tarura) baadhi ya watu wamezila.

Mongella alisema kuna tatizo ndani ya jiji kwa baadhi ya madiwani kushindwa kutekeleza wajibu wao, kusaidia maendeleo na jambo hilo limekuwa la kihistoria kwani katika jiji la Arusha hakuna Mkurugenzi aliyewahi kumaliza miaka mitatu tangu miaka ya 1980.

Alisema hana mpango wa kugombea nafasi za ndani ya chama wala uchaguzi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Serikali 2025 kama ambavyo kuna watu wanafikiri na kumfuata kumshauri afanye hivyo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad