HABARI ya mjini kwa sasa ni mshambuliji wa Geita Gold George Mpole baada ya kufunga bao lake la 17 kwa msimu uliomalizika na kuibuka kinara wa mabao huku akimpiku Fiston Mayele wa Yanga aliyekuwa na 16. Sasa amefunguka ishu yake na Simba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mpole ambaye ni mchezaji wa zamani wa Mbeya City, Polisi Tanzania na Majimaji alisema amepokea ofa nyingi kutoka timu za ndani na nje ya nchi zikitaka kumsajili lakini kwa Tanzania Simba ndio wako moto kumtaka.
Mwanaspoti linajua Simba inaweza kumsainisha muda wowote wiki hii, ilianza mazungumzo naye tangu mwanzoni mwa mwezi Juni, walipokutana faragha baada ya mechi ya Taifa Stars na Algeria akitokea kambi ya Stars.
Mazungumzo hayo baina ya Simba na Mpole hayakukamilika kutokana na ofa nyingine kubwa alizokuwa akisikilizia kutoka DR Congo, Uturuki na Morocco lakini nazo hadi sasa hakuna aliposaini mpaka kufikia jana.
“Kuna ofa zipo nyingi tu lakini sijasaini popote, nilihitaji kwanza kutimiza malengo ya msimu huu kisha ndiyo hayo mengine yafuate,”alisema.
“Simba ni miongoni mwa timu nilizowasiliana nazo lakini hatujamalizana, naamini siku si nyingi kila kitu kitaenda sawa na mtajua Mpole nitakuwa wapi msimu ujao,” alisema Mpole.
Taarifa za ndani lilizonazo Mwanaspoti ni kwamba Mpole msimu ujao atacheza Simba kwani wameshaafikiana mambo mengi na mkataba ni miaka miwili hivyo bado yeye kusaini tu.
Vigogo wa Simba jana walikuwa wakipambana kuhakikisha ishu ya mchezaji huyo inamalizika kwani Azam nao wanatajwa kumuwania pamoja na Singida Stars.
Uongozi wa Geita kupitia kwa Katibu mkuu wa Bodi,Zahra Michuzi alieleza kuwa timu hiyo haitakuwa na pingamizi la Mpole kuondoka kikosini hapo kama mwenyewe atahitaji kwenda kutafuta malisho mapya.
“Tumeshafanya naye mazungumzo lakini kama akipata ofa nzuri na akachagua kuondoka basi tutampa baraka zote na tutakachokifanya ni kutafuta mbadala wake. Tuna wachezaji wengi pia uongozi imara hivyo akiondoka Mpole mmoja tutaongeza kina Mpole watatu,” alisema Zahra.
Akizungumzia msimu wake, Mpole alisema; “Haikuwa rahisi, msimu ulikuwa mgumu pia kulikuwa na kupanda na kushuka. Lengo kuu ilikuwa kuitumikia timu kuhakikisha tunafika malengo na imekuwa hivyo.”
“Mwanzo sikuwaza kuwa mfungaji bora lakini kadri nilivyozidi kufunga wazo hilo lilinijia na baadae nikazidi kulifanyia kazi na namshukuru Mungu hatimaye imetimia,” alisema Mpole ambapo jana Mayele aliposti kwenye akaunti yake akimpongeza na kumtakia kila la heri.