KINARA wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2021/22, George Mpole amesema tuzo hiyo itamuongezea heshima na kumpa thamani kubwa katika dirisha la usajili lililofunguliwa leo.
Akizungumza na Spotileo, mshambuliaji huyo wa Geita Gold amesema haikuwa rahisi kwake kufikia mafanikio hayo na ilimbidi kujitoa ili kuweka rekodi hiyo.
"Bado sijajua msimu ujao nitacheza wapi lakini tuzo hii ya ufungaji bora imeongeza thamani yangu kuelekea dirisha kubwa la usajili, sababu huu ni muda wa kuvuna kile nilichopanda," amesema Mpole.
Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao 17, amewashukuru wachezaji wenzake na benchi la ufundi chini ya Kocha Fred Minziro kwa kumwamini na kumpa nafasi.
Mpole pia amempongeza mpinzani wake Fiston Mayele wa Yanga kwa ushindani aliomwonesha kipindi chote.
Klabu za Azam, Simba na Yanga zinatajwa kumwania mshambuliaji huyo kutokana na uwezo aliouonesha msimu huu katika umaliziaji.
Rekodi hiyo ya Mpole inamfanya kuwa mshambuliaji wa pili mzawa kuibuka kinara wa mabao katika misimu ya hivi karibuni ambapo msimu uliopita alikuwa John Bocco aliyefunga mabao 16.
Dirisha la usajili kwa klabu za Ligi Kuu ya NBC, Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite msimu wa 2022/2023 limefungliwa leo na litafungwa Agosti 31, 2022.