KLABU ya Yanga inatarajia kufunga usajili wake kwa kumsajaili mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Simon Msuva kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Simon Msuva.
Kwa mujibu wa rais mpya wa klabu ya Yanga, Hersi Said, akizungumza kwa mafumbo, alisema watafunga usajili kwa kumrejesha mtoto wao nyumbani.
Hersi alisema wanafanya usajili kulingana na mapendekezo ya kocha mkuu Nesredine Nabi kwa mchezaji wanayewahitaji akiwemo Msuva ambaye ni mzawa anayerudishwa Yanga.
Hersi alisema hayo juzi katika uchaguzi mkuu wa Yanga, baada ya kutangazwa kuwa rais wa klabu hiyo na kumtambulisha kiungo, Geal Bigirimana.
Utambulisho huo, uliwafanya Yanga kufikisha wachezaji watatu ambao imewatambulisha hadi sasa wakiwamo, Lazarous Kambole na Benard Morrison.
Hersi alisema usajili uko vizuri kwa asilimia kubwa wamekamilisha kila kitu na zimebaki nafasi chache ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ikiwamo kukamilisha usajili wa mchezaji mzawa.
"Kila kitu kipo vizuri, tayari usajili umekamilika kwa asilimia kubwa na baadhi ya nafasi tunakamilisha, kuhusu mchezaji mzawa, hilo tumefanya kile alichokipendekeza kocha Nabi, kwa kumrejesha mtoto wetu nyumbani (Msuva) waliosema harudi niwahakikishie kwamba mtoto anarudi kwao,” alisema Hersi.
Mbali na Msuva, Hersi alisema muda wowote kuanzia sasa watatambulisha mchezaji mwingine mwa kimataifa (beki wa kushoto Joyce Lomalisa Mutambala) kuwa sehemu ya wachezaji watano wa kigeni waliosajiliwa kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu hiyo.
Mutambala anajiunga Yanga akitokea Bravos do Maqui ya Angola, pia amewahi kucheza GD Interclube (Angola), AS Vita (DR Congo) na Mouscron ya Ubelgiji.
Alisema wanasajili wachezaji wazuri na ndio maana wamemchukua mchezaji wa zamani wa klabu ya Newcastle iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu nchini England.
“Sisi tunasajili na tumeahidi kabisa kushusha vifaa, huyu hajacheza timu ndogo bali amecheza timu kubwa na kwenye ligi kubwa. Wanasema eti Fiston Mayele ataenda Kaizer Chiefs, sisi wenyewe tunachukua wachezaji kwao huko," alisema Hersi.
Alisema kuna mchezaji walimtambulisha na mwingine ataingia leo Jumatatu kutambulishwa rasmi kwa sababu wanahitaji kuimarisha timu hiyo kwa msimu ujao.
“Yule mchezaji (Stephen Aziz Ki) anasubiriwa na Wanayanga niwahakikishie anatua nchini kesho Jumatatu (leo) na kuwa sehemu ya usajili ambao tumefanya kwa wachezaji ambao wametakiwa na Kocha Nabi kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu yetu.”