MTU WA MPIRA: Manara alipaswa kuwajibishwa kitambo, TFF wamechelewa sana



HATIMAYE Msemaji wa Yanga, Haji Manara amefungiwa kujihusisha na soka kwa muda wa miaka miwili na faini ya Sh2 milioni. Ilikuwa ni jambo la muda tu kufahamu kama nyakati hizi zitatokea kwa Manara.

Sio kwa sababu ya kugombana na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pale Arusha. Hapana. Ni kwa sababu ya matendo yake.

Kwa nyakati tofauti Manara amekuwa akifanya matendo ambayo sio ya kiungwana kwa watu wa soka.

Nani amesahau ugomvi wake na Shaffii Dauda? Ilikuwa ni ugomvi mkubwa. Manara alifanya kila alichojisikia kuchafua brandi ya Dauda. Nani alijali? Hakuna. Mambo yakamalizwa kienyeji tu na maisha yakaendelea.


 
Nani amesahau alivyomdhalilisha Prisca Kishamba wa Clouds TV mbele ya Waandishi wa Habari tena kwenye mkutano ambao ulikuwa mbashara kwenye TV? Hakuna.

Wanasheria waliingilia kati wakitaka Manara awajibishwe kwa kitendo kile kisichokuwa cha kiungwana. Lakini mambo yalimalizwa kienyeji na maisha yakaendelea.

Siku zote Manara amekuwa akijiona kuwa na haki ya kukosea watu wengine. Kuwadhalilisha na kuwakebehi lakini maisha yakaendelea.


Kila mtu amekuwa akiyaona matatizo ya Manara lakini walikaa kimya kwa kigezo cha kuwa mashabiki wa timu fulani.

Alipowadhalilisha waandishi wa habari, mashabiki na wadau wengine walikuwa upande wake. Wakadai waandishi wa habari ni ‘watu wa ovyo’ na wanapaswa kufanyiwa yale wanayofanyiwa.

Au mmesahau alivyoanza kuwashambulia na kuwadhalilisha viongozi wa Simba mara baada ya kuamua kuachana naye? Hapana. Watu wa Yanga walichekelea kwa kuwa wanadhalilishwa viongozi wa Simba.

Ametoa tuhuma nyingi dhidi ya Simba. Ametoa tuhuma nyingi dhidi ya mwekezaji wa Simba. Nani alijali? Hakuna.


 
Ikafika hatua Manara akaonekana ni mkubwa kuliko Simba na Yanga. Akaonekana ni mkubwa kuliko Waandishi wa Habari na hata vyombo vyao. Alifanya kila alichojisikia na hakuona kama kuna mtu wa kumgusa.

Mwaka jana tu hapo alipewa onyo na faini kwa makosa hayo hayo. Kuna siku aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuituhumu TFF pamoja na Bodi ya Ligi wanaumiza timu yake.

Akapelekwa kwenye Kamati ya Maadili na kupigwa faini. Akaenda kulipa faini kwa ‘majigambo’ tena akichukuliwa na vyombo vya habari. Ilikuwa ni ishara kama anaona fahari vile kukosea. Inafikirisha sana.

Mwishowe ukubwa wake ukataka kupitiliza. Akaonekana akigombana na viongozi wakubwa wa TFF hadharani. Tena kwenye Jukwaa Kuu ambalo lilikuwa na viongozi wakubwa tu wa Serikali.


Akagombana mbele ya wafadhili wa Yanga na viongozi wengine wakubwa wa mpira. Kwa nini? Ni kwa sababu alishaona hakuna wa kumgusa. Ni kwa sababu alishaona pengine yeye ni ‘mkubwa’ kuliko hata TFF yenyewe. Ila tuelewane, hakuna aliyekamilika na pengine Karia alimzingua kweli, lakini bado alipaswa kulinda heshima na ustaarabu wa soka. Mchezo wa kistaarabu!

Ni changamoto ya kuacha matatizo madogo yakue mwishowe akagombana hadi na watu wenye dhamana ya soka letu.

Pengine watu hawafahamu kitu. Rais wa TFF ndiye kiongozi wa juu kabisa wa soka Tanzania. Ni mtu mwenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi.

Huwezi kumsema vibaya mbele ya hadhara ya watu. Huwezi kumtolea maneno ya kashfa mbele ya hadhira ya watu.

Kwanza, unakuwa umeidhalilisha taasisi iliyoaminiwa kuongoza mpira wa nchi. Pili unakuwa umemkosea heshima rais mwenyewe wa shirikisho. Huku ni kukosa adabu kulikopitiliza.


 
Unapokuwa kwenye familia ya soka, lazima uheshimu viongozi wako. Unapokuwa katika taasisi lazima uheshimu wenye mamlaka zaidi yako.

Pia, unapaswa kuheshimu hadi watu wadogo kwenye taasisi hizo.

Lakini busara hii aliikosa Manara pale Arusha. Haijalishi kilitokea kitu gani, lakini alipaswa kuwaheshimu watu wenye mamlaka zao.

Rais wa TFF sio mtu ambaye unaweza kumtolea maneno kama yale yaliyotajwa na Kamati ya Maadili.

“Umekuwa ukinifatafata sana, huna cha kunifanya na ninaweza kukufanya chochote.” Ni maneno yaliyokosa busara na heshima, kama ni kweli aliyatamka kwenye mzozo wao!

Hebu fikiria katika matukio yote makubwa ya kimichezo nchini ambayo ataitisha Rais wa nchi, huwezi kukuta Rais wa TFF hajaalikwa. Sio tu kualikwa, atapewa na nafasi ya kuzungumza.

Hii ni ishara kuwa huyu mtu ana heshima kubwa sana katika nchi. Ni ishara kuwa hata serikali inatambua anachofanya na kumsimamia. Ndio sababu Rais wa TFF akikosea chochote katika ofisi yake, serikali inaweza kumwajibisha. Kumbuka yaliyotokea kwa Jamal Malinzi.

Hivyo, watu wanaomtetea Manara waache unafiki. Walipaswa kumwambia ukweli mapema. Asiwe mtu wa kujikweza na kudhalilisha wengine. Hiyo sio busara ya watu wenye heshima kubwa kwenye soka la nchi hii kama yeye.

Kuna baadhi wanadhani Manara amefungiwa kwa kuwa ni mtu wa Yanga. Hakika huu ni ujinga uliopitiliza. Wamesahau Manara akiwa Simba aliwahi kufungiwa mwaka mmoja na faini ya Sh9 milioni? Pengine binadamu wanasahau haraka.

Katika nyakati hizo Manara anafungiwa akiwa Simba, Jerry Muro aliyekuwa Yanga naye alifungiwa. Ni kwa sababu walivuka mipaka yao.

Hili la kufungiwa sasa linapaswa kumfundisha adabu zaidi.

Anaweza kuona yupo sawa kwa sasa, kumbe anaharibu hata mambo mengine mazuri ambayo angeweza kupewa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad