Mtumbuizaji wa Tiktok wa Kenya ametoa wito kwa watu wamuombee baada ya mapishi aliyotengeneza kumharibikia.
Aq9ine ambaye huwatumbuiza wanamitandao kwa kujaribu vyakula mbalimbali vya ajabu anaugua baada ya kula buibui.
Jumamosi asubuhi mwanatiktok huyo alipakia video ya kutisha inayoonyesha uso na mikono yake ikiwa imevimba vibaya.
"Ikiwa hii ndio video yangu ya mwisho, imekuwa jambo la kufurahisha kuwaburudisha na kuhatarisha maisha yangu pia. Ninapenda hatari sababu tunaishi hatari. Sisi sote tutakufa. Nawapenda sana ndugu zangu," Aq9ine aliandika chini ya video hiyo ambayo alipakia kwenye Instagram.
Katika video hiyo mwanatiktok huyo alielezea dalili alizokuwa nazo huku akionyesha jinsi mwili wake ulivyoathirika.
"Wadau,, nifanyieni maombi ya mwisho kabla niende. Mniombee tu bana mi naenda. Nasikia ni kama sina uso, nafura tu. Mazee nimekula buibui bana. Hii inafanyikia uso wangu. Nifanyieni maombi ya mwisho," Alisema kwenye video.
Aq9ine alionekana mwenye maumivu makali na wasiwasi mwingi. Pia alishinda akijikuna kwenye uso na mikono.
Video yake ilialika hisia mseto kutoka kwa wanamitandao huku wengi wao wakimtakia afueni na wengine wakimkosoa.
Aq9ine hata hivyo alionekana kukerwa na waliochukua hatua ya kumkosoa na kumshauri dhidi ya sanaa yake.
"Mnaboo bana. Mnakasirika juu ya shida zangu mbona?. Mimi nikikufa nitazikwa na mnisahau. Haufai kushtuka juu mimi si wenu," Aliandika kwenye Instastori zake.
Aidha mtumbuizaji huyo ameapa kuendelea kupika na kula wanyama zaidi, akianza na chura na nyoka pindi baada ya kupata afueni
"Uzuri yangu sitawai wapostia Till mnichangie pesa za hospitali. Bora mniahidi nikifa mtakuja kwa mazishi yangu Kenya nzima na msaidie familia yangu kupanga mazishi," Alisema.
Tazama:
Haya yanajiri siku chache tu baada yake kufichua kuwa aliugua baada ya kupika na kula popo, shughuli ambayo alionyesha kwa video.
Mapema mwezi huu Aq9ine akiwa kwenye mahojiano alifichua kuwa aliugua vibaya siku nne baada ya kula popo.
"Baada ya siku nne baada ya kukua bat, nilishikangwa na kihoma, pua inayokimbia kwa saa sita ..." Alisema katika mahojiano na Presenter Ali.
Mtumbuizaji huyo alisema alitumia aina yingi tofauti za dawa katika juhudi za kutafuta tiba ila hakuna iliyofanya kazi.