Mugalu: Mjipange narudi upya




STRAIKA wa Simba, Chris Mugalu hakuwa na bao hata moja msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, licha ya kupata nafasi za kucheza.

Aliposajiliwa Simba kabla ya msimu uliopita aliweka rekodi ya kumaliza msimu akiwa na mabao 15, nyuma bao moja kwa John Bocco aliyeibuka Mfungaji Bora akiwa na mabao 16.

Mugalu alionyesha kiwango bora hadi kwenye mashindano mengine ambayo Simba ilishiriki, lakini msimu uliopita hakufanya hivyo, ingawa kuna nyakati hakucheza kutokana na majeraha yaliyomuandama.

Baada ya msimu kumalizika, nyota huyo alirejea kwao kwa ajili ya mapumziko na sasa yupo kambini na wenzake nchini Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.


 
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Mugalu anaelezea mambo mbalimbali hasa aliyokumbana nayo msimu uliopita na kushindwa kufunga bao hata moja.

Anasema sababu kubwa ni majeraha ya mara kwa mara aliyopata hadi kushindwa kucheza michezo mingi mfululizo.

“Hata mechi nilizokuwa uwanjani sikuwa sawa kwa maana ya utimamu wa mwili kwenye hali ya ushindani. Pengine ndio maana nilikutana na changamoto ya kugongana na mwenzangu uwanjani nil iumia tena,” anasema Mugalu.


“Sikupata nafasi ya kucheza mfululizo dakika nyingi jambo ambalo lilikuwa changamoto kwangu ndio maana kwenye mashindano mengine niliyopata muda wa kucheza nimefunga mabao.”

Anasema akiwa FC Lupopo ya DR Congo aliwahi kukutana na changamoto kama hiyo ya kucheza msimu mzima bila kufunga bao lolote kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.

Mugalu anasema msimu uliofuata alionyesha makali kwa kumaliza mfungaji bora wa msimu hadi kupata ofa za kuhitajika na timu nyingine mbalimbali ikiwemo FC Lusaka iliyofanikiwa kupata saini yake.

“Hali hii ya kutofunga hapa Tanzania sio kama nimependa, bali ni changamoto ya majeraha niliyokutana nayo mfululizo,” anasema.


 
Anasema klichomsumbua ni tatizo la nyama za nyuma ya paja kumuuma mara kwa mara kutokana na kupenda kucheza kwa nguvu kushindana na mabeki wa timu pinzani ili kuhakikisha anaisaidia timu yake au kufunga mabao.

“Nikipata muda wa kupumzika na matibabu mazuri huwa napona na kurejea haraka uwanjani, ila muda mwingine huwa zinanisumbua kama ilivyo wakati huu, lakini naamini nitakuwa sawa na kurudi kwenye ushindani,” anasema Mugalu aliyefunga mabao mawili kwenye Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

HATIMA YAKE

Mugulu bado ni mchezaji wa Simba kwani ana mkataba, lakini amekuwa akihusishwa kuondoka ndani ya timu hiyo kutokana na ofa anazodaiwa kupata.

Hata hivyo, bado viongozi wa Simba wamegawanyika juu ya uwepo wake ndani ya klabu hiyo, kwani kuna wanaotaka aondoke na wengine wanatetea abaki wakiamini ni mchezaji mzuri hata kama msimu uliopita hakufunga bao lolote.


Mugalu anasema hana wasiwasi wowote na hatma yake ya msimu ujao kwani ni mchezaji wa Simba maana mkataba wake umebaki mwaka mmoja.

“Naamini katika uwezo wangu. Msimu ulioisha ni changamoto tu za majeraha hadi kushindwa kufanya vizuri, kama nikibaki hapa nitarudi kwenye makali yangu au nikiondoka nitaenda kuonyesha ubora huko.

“Maisha ya mchezaji soka ndio yalivyo unaweza kuwepo kwenye timu ama ukaondoka. Hapo sina wasiwasi na lolote kati ya hayo mawili kuondoka ama kubaki, kwani naamini kwenye uwezo wangu.”

Inaelezwa mabosi wake wamepokea ofa tano kutoka timu mbalimbali zikitaka huduma yake zikiwamo Zesco United, Nkana Red Devils, Power Dynamos zote za Ligi Kuu ya Zambia na FC Saint-Eloi Lupopo ya Ligi Kuu ya DR Congo.

MKATABA UKOJE

Alipojiunga Simba Agosti 2020 akitokea Dynamos, nyota huyo alisaini mkataba wa miaka miwili ambao ndani yake ulikuwa na nyongeza ya mwaka mmoja na kuwa mitatu, hivyo umebaki mwaka mmoja.


 
Simba iliongeza mkataba wa mwaka mmoja kutokana na kuridhishwa na kiwango chake msimu wake wa kwanza.

Mugalu anasema aliongeza mkataba wa mwaka mmoja akiwa ndani ya mkataba wake wa miaka miwili.

“Kuna timu hizo nne kweli zimeonyesha nia ya kunihitaji, ila nimewaeleza wote kuwa nina mkataba mrefu na Simba siwezi kufanya uamuzi wowote kwa sasa kuhusu hatma yangu ya msimu ujao,” anasema.

MSIMU ULIOPITA

Mchezaji huyo anasema miongoni mwa mambo yanayomtesa wakati huu ni kushindwa kufanya vizuri sio katika Ligi Kuu Bara pekee, bali hata mashindano mengine.

Anasema aliweka malengo ya kuendeleza kile alichofanya msimu wa kwanza ndani ya Simba, lakini bahati mbaya kwake alishindwa kufikia malengo hayo.

“Kuna muda huwa nakaa chini au hata wakati wa kulala jambo hilo huwa linarudi katika akili yangu, kama ndoto vile, yaani nashindwaje kumaliza msimu bila kufunga bao, ila ndio changamoto na tayari imetokea. Nitalifanyia kazi,” anasema.

“Niombe radhi mashabiki wa Simba na wale wanaonipenda, halikuwa lengo langu, bali ni changamoto ambazo hazikuwa ndani ya uwezo wangu kuzizuia. Msimu ujao nitapambana ili kufanya vizuri na kuwafuta machozi yao.”

SIMBA IJAYO BALAA

Akiizungumzia Simba, Mugalu anasema iko vizuri na itashangaza. “Ukiangalia msimu uliopita kuna maeneo tulishindwa kufanya vizuri pengine ilikuwa sababu ya kushindwa kufikia malengo tuliyojiwekea mwanzoni mwa msimu,” anasema.

“Tunakwenda kufanya maandalizi ya kutisha ili msimu ujao turudi katika ubora.”



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad