Pambano hilo ni fursa ya kupanda kwenye renki kwa Mwakinyo ambaye tangu Septemba mwaka jana alipomchapa Julius Indongo, hajawahi kuonekana ulingoni.
Kama atashinda, Hassan Mwakinyo ataandika historia mpya kwenye ndondi duniani, katika pambano lake la Septemba 3.
Mwakinyo sasa atazichapa na bondia namba moja nchini Uingereza, Liam Mark Smith pambano la raundi 12.
Smith bondia wa nyota tano aliyefungiwa kucheza Marekani anakamata nafasi ya sita duniani kwenye uzani wa super welter ambako Mwakinyo ni wa 37 kwa sasa baada ya kuporomoka hivi karibuni akiwa na nyota tatu na nusu.
Endapo atashinda, bondia huyo namba moja nchini ataandika rekodi mara dufu kushinda ile ya 2018 alipomchapa Sam Eggington aliyekuwa bondia namba nane wa dunia kwenye uzani huo, pambano lililompandisha hadi nafasi ya 14 duniani kwenye uzani wake kabla ya kuporomoka kwa kutocheza muda mrefu.
Juzi kocha wa Mwakinyo, Hamis Mwakinyo ambaye pia ni kaka yake aliiambia Mwananchi Digital kuwa bondia huyo amerejea nchini akitokea Marekani alikokuwa akiishi kwa miezi kadhaa.
"Yuko kwenye maandalizi ya kucheza pambano kubwa," alisema kocha huyo ambaye pia ni kaka yake.
Tayari pambano hilo limewekwa kwenye ratiba ya mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) na limepangwa kuwa la raundi 12.
Mwakinyo atapanda ulingoni akizidiwa ubora, rekodi na uzoefu na mpinzani wake ambaye amepigana mapambano 35 na kushinda 31, amepigwa mara tatu na kutoka sare mara moja tangu 2008.
Mwakinyo yeye amepigana mapambano 22, ameshinda mara 20 na kupigwa mara mbili tangu 2015.