Mtwara. “Huu ni msiba mkubwa kwetu. Tunafunga shule kesho Alhamisi Julai 28 lakini kwa mazingira yalivyo tumesimamisha kuendelea na masomo kuanzia leo (jana).”Maneno ya Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi King David ambayo wanafunzi 11 wamefariki katika ajali ya basi la shule iliyotokea jana katika eneo la Mjimwema, Kata ya Mikindani, Mtwara Mjini.
Kwa mujibu wa ratiba, shule zote nchini zitafungwa kesho na Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Daniel Msilu akizungumza na Mwananchi “shule zilikuwa zinafungwa keshokutwa (kesho) lakini sisi tutafunga kwa stahili ya huzuni.”
Amesema shule hiyo yenye madarasa ya awali hadi darasa la saba imechukua uamuzi wa kuwarejesha nyumbani ili kutoa fursa ya kuomboleza msiba huo mkubwa.