Riaan Swiegelaar; ni mwanzilishi mwenza wa Kanisa la Kishetani la Afrika Kusini
Riaan Swiegelaar; ni mwanzilishi mwenza wa Kanisa la Kishetani la Afrika Kusini ambaye ameamua kuokoka na kuachana na kanisa lake hilo baada ya kudai kuoneshwa upendo usio wa kawaida na kukutana binafsi na Yesu Kristo.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Riaan anasema kwamba alitamani kuachana na kanisa hilo kimyakimya kwa sababu hakufikiria kama watu wa kanisa hilo wangefurahishwa na uamuzi wake wa kuondoka na kufuta uanachama wake ndani ya kanisa hilo la South African Satanic Church (SASC).
Riaan anaeleza kuwa alijiunga na kanisa hilo la SASC wakati ambao alikuwa na hali mbaya kiuchumi anasema alijihusisha na mambo mengi yaliyokuwa yakifanywa katika kanisa hilo la kishetani.
Riaan anasema kuwa, mwezi Mei 2022, alihojiwa kwenye kituo cha redio cha Cape Town ambapo alitangaza kuwa haamini kuwepo kwa Yesu Kristo.
Lakini sasa anasema kuwa, baada ya mahojiano hayo, mfanyakazi mmoja wa kike kutoka kituo hicho cha redio alimsogelea na kumkumbatia kwa namna ambayo hajawahi kukumbatiwa hapo awali.
“Alinigusa na kuniambia maneno mazuri kwa namna ambayo sijawahi kuambiwa nilijihisi kupendwa hasa kwa kitendo cha mfanyakazi huyu wa redio alivyofanya.
“Wiki moja baadaye, niliwasiliana naye kupitia WhatsApp na akaniambia kuwa yeye ni Mkristo na kunishuhudia kuhusu Yesu Kristo na jinsi anavyoweza kubadili maisha yangu.
“Nilifurahi sana kwa upendo alionionesha na kunipokea bila kunibagua. Hilo lilibaki kwangu kuwa ni jambo kubwa katika maisha yangu,” anasema Riaan.
Stori: Sifael Paul