MZEE mwenye umri wa miaka 89, Iddy Maganga, ameamua kuvunja nyumba zake mbili zenye thamani ya Sh. milioni 200, eneo la Ngarenaro NHC jijini Arusha kwa madai baadhi ya watoto wake wanataka kumdhulumu ili wazimiliki.
Akizungumza katika mahojiano na Nipashe, Mzee Maganga alisema katika kutekeleza kile alichokiita mpango wa kutaka kumuua, mmoja wa watoto wake alimfungia ndani kwenye chumba chenye giza nene kwa muda wa wiki moja, bila kumpa chakula wala mahitaji muhimu na kulazimika kula kinyesi chake.
Maganga alisema nyumba zake alizijenga na mke wake ambaye alishafariki dunia.
"Niliamua kuzivunja nyumba hizo kwa kukodi watu ambao niliwalipa baada ya kubaini kwamba baadhi ya watoto wangu wakiongozwa na Abdalah Maganga wanania ovu juu ya mali zangu," alisema.
Aliongeza kuwa alichukua uamuzi huo akiwa na akili timamu na amefanya hivyo ili kuwakomesha watoto wasiotaka kufanya kazi, wakisubiri mali za urithi kutoka kwa wazazi wao.
"Hii nyumba ni mali yangu, nilijenga na mke wangu ambaye kwa sasa ni marehemu, huyu mtoto Abdalah alinifungia ndani wiki moja nikiwa nakula kinyesi changu sijitambui na nilikuja kuokolewa na mtoto wangu wa kike aitwaye Jasimin na mume wake baada ya kuvunja kitasa na kunitoa na kunipeleka hospitali," alisema.
Akisimulia zaidi, alisema jirani yake aliyemtaja kwa jina la mama Masawe ambaye alikuwa akienda kuchukua chakula kwake, alimpigia simu mtoto wake Jasimin na kumwambia kuwa mzee Abdalah haonekani siku ya nne.
Baada ya taarifa hizo, binti yake na mume wake walikwenda nyumbani na kumkuta akiwa amefungiwa ndani hajitambui kutokana na njaa.
Mzee Maganga mwenye watoto sita, kwa sasa anaishi kwa mtoto wake eneo la Kwa Mrombo, akidai kuwa Abdalah alikuwa na nia mbaya juu yake, kutaka afariki dunia ili ajimilikishe nyumba hiyo kinyume cha sheria.
Alisema, licha ya kuwa hiyo nyumba ni mali yake, lakini mtoto wake alikuwa hamruhusu baba yake kuingia ndani ya nyumba hiyo na anapokuwa akitaka msaada kwa kijana huyo, alikuwa akifunga milango na geti.
Mzee Maganga aliwataka Abdalah na Mwenzake Ridhiki Maganga kukaa mbali na mali zake wakatafute mali zao na kwamba baada ya kubomoa nyumba hiyo ana mpango wa kuliuza eneo hilo.
"Baada ya kupata fahamu nilianza taratibu za kuuza nyumba yangu, lakini kila nikifika na mteja nafungiwa nje na mwanangu Abdalah, hataki niingie ndani hata kujisaidia," alilalamika.
Jasimin, akizungumzia tukio hilo la baba yake, alisema alimwokoa akiwa kwenye hali mbaya baada ya kumkuta hajitambui na amefungiwa kwenye chumba kidogo kwa wiki moja bila kupatiwa chakula wala maji.
"Nilimkuta baba yangu akiwa kwenye hali mbaya sana alikuwa haongei, chumba kilikuwa na giza kimefungwa na kinanuka kinyesi na alikuwa akila kinyesi chake, nilimpeleka hospitali na baada ya kupatiwa matibabu alipata nafuu na kurejea katika hali ya kawaida na sasa naishi naye," alisema.
Mtoto anayetuhumiwa kufanya tukio hilo, Abdalah Maganga, alikanusha taarifa za kumfungia baba yake kwenye chumba kwa wiki nzima bila chakula, akidai kuwa taarifa hizo hazina ukweli.
Abdalah alikiri kuwa nyumba hiyo ni mali ya baba yake na marehemu mama yake na yeye alikuwa akiishi hapo kama mwangalizi.
Alisema ameshtushwa kuona kundi la watu zaidi ya 50 kuvamia nyumba hiyo siku ya Jumamosi wiki iliyopita na kufanya uharibifu.
Alisema baada ya kundi hilo kuvamia alijitahidi kutafuta msaada polisi, lakini hakupata kwa wakati na walipofika kwa kuchelewa walikuta nyumba zote zimevunja na vitu kutolewa nje.
"Mimi sina ugomvi na baba yangu ila sina mawasiliano naye kwa muda baada ya kuchukuliwa na kuishi na mdogo wangu Jasimin, nitakachofanya kwa sasa ni kumwachia Mungu tu," alisema Abdalah.
Hata hivyo, mdogo wake Mzee Maganga, Hasan Abdalah, alisema hana mawasiliano na kaka yake na kushauri kuwa kitendo kilichotokea kinapaswa kumalizika kisheria mahakamani.