NAIBU Rais William Ruto jana Ijumaa alimkaripia vikali Rais Uhuru Kenyatta akisema, hana shukurani kwa kumwandama kisiasa baada ya kumsaidia kutwaa mamlaka.
Huku akidai kuwepo njama za kumwangamiza yeye na watoto wake, Dkt Ruto aliambia umati katika eneo la Kapsabet, Nandi kwamba, Rais Kenyatta amesahau upesi alivyomwezesha kushinda urais 2013 na 2017.
“Nilikusaidia ulipohitaji mtu wa kukusaidia. Ikiwa hutaki kuniunga mkono, achana na mimi. Kwa heshima kuu, Bw Rais kuwa mwadilifu. Kuwa mtu muungwana. Kuwa na shukrani. Sisi ndio tulikusaidia. Na sasa unaanza kunitishia, eti utanifanyia nini. Bora usiue watoto wangu lakini mimi na wewe tafadhali tuheshimiane,” alifoka Naibu Rais.
Dkt Ruto alisema kwamba, Rais Kenyatta badala ya kumhangaisha anapaswa kujishughulisha na kampeni za mpeperushaji bendera wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya, Raila Odinga, anayempigia debe.
Alimkashifu Kiongozi wa ODM kwa kusababisha fujo kila baada ya uchaguzi nchini, ikiwemo kujiapisha kama rais jinsi ilivyoshuhudiwa katika chaguzi kuu zilizopita.
“Nataka nimwambie Rais, wacha kuniletea maneno rafiki yangu. Wewe si una candidate wako Bw Kitendawili. Unaniongelea nini? Wacheni kuzungumza kunihusu, zungumzeni kumhusu mgombeaji wako. Utuambie huyu mtu wa kitendawili atawacha kung’oa reli lini? Atawacha kujiapisha lini? Atawacha kuvuruga Kenya lini? Atawacha mambo ya fujo lini na utuambie ajenda ya huyo jamaa. Wachana na William Ruto,” akasema.
Mchanganuzi wa siasa, Kipchumba Karori asema, matamshi ya Naibu Rais yalishinikizwa na mkutano wa faragha uliofanyika Jumatano kati ya Rais Kenyatta na wazee wa jamii ya Kalenjin.
Bw Karori alidai kuwa kambi ya Azimio imedhihirisha kuwa itafanya kila iwezalo kuhakikisha Dkt Ruto haingii ikulu.
Akizungumza na Taifa Leo, alipuuzilia mbali madai kuwa Naibu Rais amejawa na machungu na hasira, akisema ni propaganda zinazoenezwa na wapinzani wake ili kumsawiri vibaya kwa Wakenya.
“Ruto hakuwa na hasira. Alikuwa tu akirejelea yale waliyoambiwa wazee wa jamii ya Kalenjin. Ikiwa mtu anaweza kuwatishia wazee wa jamii, je atamfanyia nini Ruto? Alisema hayo kuashiria uzito wa vitisho anavyopatiwa ikizingatiwa Uhuru aliwahi kusema Ruto hatakuwa debeni. Ni muhimu kukumbuka mamlaka hayapeanwi, hutwaliwa kwa nguvu. Tunazungumzia kuhusu viongozi ambao wamechukulia Kenya kama mali yao na wako tayari kufanya lolote,” alisema Bw Karori.
MFUMO WA UCHUMI
Kulingana na mchanganuzi huyo, uchaguzi ujao unahusu mfumo wa uchumi ambao Wakenya wangetaka, kupitia wagombea wa urais watakaowachagua.
Lakini Bw Mark Bichachi, ambaye vilevile ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, anasema matamshi ya Naibu Rais yanadhamiriwa kuvutia huruma kutoka kwa wapiga kura.
Huku akitaja matamshi hayo kama uchochezi, Bw Bichachi alisema kuwa kiongozi huyo wa Kenya Kwanza anafahamika kwa visa vyake vya kuchochea hisia za Wakenya.
“Ruto anataka kuvutia huruma tu. Unakumbuka majuzi akisema watu 117 wameuawa kwa sababu ya serikali kumwandama? Kila mara anatafuta huruma licha ya kumtukana Rais na kumwita tapeli mara kwa mara. Matamshi yake ni uchochezi mtupu na yanayolenga kuchochea hisia za watu ikizingatiwa ameyatoa akiwa katika ngome yake nyumbani,” alisema Bw Bichachi.
Raila alaani fujo huku wafuasi wa wagombeaji ugavana...