Pacha Wafariki Mazingira tata Dar, Wapenzi Wauawa Dom



Dar/Dodoma. Matukio ya vifo yameendelea kutikisa nchini, sasa pacha wanaodaiwa kupewa sumu wamefariki dunia jijini Dar es Salaam, huku watu wengine wawili wameuawa mkoani Dodoma kwa madai ya wivu wa mapenzi.


Pacha hao, Khalifa na Alif Ally wenye umri wa miaka 22 walifariki dunia Jumamosi iliyopita katika mazingira ya kutatanisha wakidaiwa kulishwa sumu na mwanamke aliyekuwa akiwasomea dua.


Huko Dodoma, watu hao wawili waliodaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi waliuawa kwa kile kinachodaiwa wivu wa mapenzi na mtuhumiwa anadaiwa kuwa mpenzi wa zamani wa mwanamke.


Tukio la pacha Dar


Pacha hao walifikwa na umauti kwa nyakati tofauti, ikiwa ni saa kadhaa baada ya kumuaga mama yao asubuhi ya siku hiyo kuwa wanakwenda kusomewa dua kwa mama ambaye hakufahamika jina.


Pacha hao walidai kuhisi kukabwa usiku kila wanapolala, hivyo walihitaji kufanyiwa dua.


ADVERTISEMENT

Khalifa alikuwa mwanafunzi katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Alif alikuwa mwanafunzi wa chuo cha TIA.


Akizungumza na Mwananchi, Ally Dilunga ambaye ni kaka wa pacha hao, alisema kabla ya tukio hilo, saa 2 asubuhi alipokea ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa Khalifa ukiwa na namba mbili za simu huku akiambatanishwa na ujumbe “hizo ndiyo namba za huyo mama tunapoenda.”


Alisema ujumbe huo pia uliambatanishwa na “live location” ambayo ingeweza kurahisisha mtu kujua sehemu walipo.


Baada ya kupokea ujumbe huo, alijaribu kumpigia simu na awali hakupokea na baadaye simu yake ilionekana kuwa ilikuwa inatumika, jambo lililomfanya Ally kumpigia mama yao kujua ndugu zake wanapokwenda, ndipo aliambiwa wameenda Buza Mnarani kusomewa dua.


Alisema ilipofika saa nne asubuhi alipokea simu kutoka kwa Khalifa akimwambia kuwa anaumwa sana, hali zao ni mbaya pamoja na mwenzake na kwamba wapo Buza Mnarani.


Ally alisema taarifa hiyo ilimfanya atoke alipo (Chanika) kuelekea eneo hilo na alijaribu kumpigia tena Khalifa simu, haikupokelewa ndipo alipopata wazo la kumpigia simu mama huyo na kumuomba amwelekeze, ndipo alisema akifika atamtuma mtu amfuate kituoni.


Alisema akiwa eneo la Banana, mama huyo alimpigia tena simu kumuambia mtu ameshakwenda kumpokea stendi, jambo lililomfanya kuhoji ni nani anayekwenda kwa sababu yeye hajafika eneo husika.


“Nilimuomba yule mama kuwa huyo mtu anayekwenda akifika anipigie simu niongee naye, nilipoongea naye niligundua ni Malik, rafiki wa Kulwa na Dotto ambaye ni dereva bajaji, Buza,” alisema Ally.


Alipofika Malik ndiyo alimfuata na alimpeleka kwa huyo mama na alimkuta Khalifa akiwa hana fahamu na amelala kwenye mto, huku yule mama akiwa amemshika paji la uso kwa mkono wake wa kulia huku akisoma Quran kupitia simu yake ya mkononi.


“Kulwa (Alif) alikuwa amelala katika kiti huku akiwa anatapika na kumshika mguu Dotto (Khalifa) karibu mara tatu, jambo lililonifanya nishituke,” alisimulia Ally.


Alisema alipomgusa Dotto alibaini kuwa mguu wake ni wa baridi, lakini hakutilia shaka, kwani alihisi hali ya hewa huenda imechangia.


Alisema muda huo alitoka nje kuzungumza na baba yake katika simu na aliporudi ndani alikuta yule mama akimpapasa Dotto kuanzia kifuani hadi tumboni na alipohoji alisema joto halirudi mwilini mwake.


Suala hilo lilimfanya awachukue ndugu zake hao na kuwakimbiza hospitali huku akimtaka yule mama kuongozana nao na walipofika hospitali ya Aga Khan-Buza waliambiwa waende Temeke.


Kauli ya Daktari


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Dk Joseph Kimaro alisema waliwapokea pacha hao Jumamosi huku mmoja akiwa ameshafariki dunia.


“Yule mwingine (Kulwa) alikuwa akionyesha matumaini ya kuendelea vizuri na aliweza kwenda chooni mwenyewe na kuchagua kitanda, tukawa na matumaini ataendelea vizuri, lakini hali ilibadilika ghafla na tukampoteza.


“Tulichukua sampuli za matapishi, mkojo, damu tukaikabidhi polisi, ili ipelekwa kwa mkemia mkuu kufanyiwa utafiti kujua ni kitu gani kimesababisha mauti hayo... itakuwa ni kemikali ambayo ilileta shida kwa haraka ukizingatia walikuwa ni watu wenye afya na hili limetokea ghafla,” alisema Dk Kimaro.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema upelelezi unaendelea.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad